Na Mathias Canal, Rombo
Kikundi cha Upendo Group kutokea nchini Israel kimewasili katika Wilaya ya Rombo kwa wiki mbili kuanzia tarehe 26 Julai 2022 mpaka tarehe 6 Agosti 2022.
Pamoja na kufanya utalii lakini kikundi hicho kitakarabati madarasa mawili ya shule ya msingi Simbalo, ujenzi wa jiko la shule, kuweka mtandao wa umwagiliaji (Drip Irrigation) kwenye kilimo cha mbogamboga kwa ajili ya wanafunzi shuleni hapo.
Watalii hao 35 wa kikundi cha Upendo Group wamekusudia kuunga mkono juhudi za serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan katika kufanya shughuli za jamii ikiwemo kuboresha miundombinu ya madarasa.
Akizungumza na wananchi katika Kijiji cha Simbalo, Kata ya KatangaraMlele mara baada ya kuwapokea waalii hao tarehe 26 Jalai 2022 Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe Prof Adolf Mkenda amewashukuru watalii hao kutoka Israel ambao wamejitolea kuendeleza juhudi za serikali katika kuimarisha sekta ya elimu.
Amesema Rais Samia Sulu Hassan ametoa fedha nyingi kwenye Wizara ya Elimu kwa ajili ya kuendeleza sekta hiyo ikiwemo fedha za UVICO 19 zilizofanya kazi nzuri kujenga madarasa 15,000 kwa shule za msingi pamoja na shule shikizi ambapo katika Wilaya ya Rombo ilipata shule shikizi moja na madarasa 44 huku kwa upande wa shule za sekondari kupitia mpango huo yamejengwa zaidi ya madarasa 20,000.
Waziri Mkenda amesema kuwa Rais Samia ametilia mkazo zaidi katika kuimarisha sekta ya elimu ambapo pamoja na juhudi zote za serikali lakini serikali haifungi milango kwa watu wenye uwezo wa kuunga mkono jitihada za serikali.
“Serikali sasa inatoa elimu bila ada haijasema wananchi kwa hiari yao wasijitolee kuendeleza sekta ya elimu, kwa wale wenye uwezo wa kujenga madarasa, kununua madawati na mengineyo ni vizuri wenye uwezo wa kuchangia juhudi za serikali waendelee kufanya hivyo” Amekaririwa Waziri Mkenda
Waziri Mkenda amesema kuwa aibu ya changamoto ya vyoo shuleni ni lazima kuimaliza. “Waziri wa TAMISEMI Mhe Innocent Bashungwa amesema ataanza kampeni ya ujenzi wa vyoo na mimi namuunga mkono na wananchi tumuunge mkono ili kuboresha mazingira ya shule ili yawe ni mahali pazuri kwa wanafunzi ili waweze kupenda kusoma” Amesema Waziri Mkenda
Waziri Mkenda ametoa mwito kwa wadhibiti ubora nchini kutoficha matatizo ya shule badala yake watoe taarifa ili serikali iweze kufanya kazi yake ipasavyo. Amesisitiza taarifa zikusanywe na kusema ukweli na uwazi wa hali halisi.
MWISHO