Home Kitaifa WANANCHI WALIOPATIWA VOCHA ZA VIWANJA WATAKIWA KULIPIA MAPEMA ILI KUPATA HATI

WANANCHI WALIOPATIWA VOCHA ZA VIWANJA WATAKIWA KULIPIA MAPEMA ILI KUPATA HATI

WANANCHI ambao wamepatiwa vocha za viwanja Mkoa wa Tanga wamekumbushwa kulipia viwanja hivyo ili wapatiwe hati kwa haraka ili kuepusha mrundikano kwakuwa huduma ya upatikanaji wa hati kwa sasa ni wa haraka.

Akiongea baada ya kukabidhi hati kwa wananchi wapatao 110, Leo Kamishna msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Tanga Tumaini Gwakisa alisema wananchi wengi wamepatiwa vocha lakini wanasuasua kulipia viwanja vyao.

Gwakisa alibainisha kwamba wana mpango wa kupeleka vituo jumuishi vya kutolea huduma katika Wilaya 11 mkoani humo kwenye maeneo ambayo wananchi wengi wamelipia ili kuepusha usumbufu kwa wananchi hao kufuata huduma hiyo ofisini kwao.

“Tuna viwanja vingi ambavyo vimepangwa na kupimwa, wananchi wamepewa vocha lakini bado hawajavilipia, ama kupitia urasimishaji au vilivyopangwa,

“Wito wangu kwao, ikiwa kama wataweza kuvilipia wote ndani ya muda mfupi, tutapeleka huduma ya vituo jumuish pale ili wote waliolipia wote wanapata hati zao pale ndani ya muda mfupi, kwahiyo wasiogope hati zinatoka” alibainisha.

Aidha Gwakisa alisema kwa Mkoa wa tanga wamewekewa malengo ya kutoa hati elfu 15 kwa mwaka huu, na kwamba wapo katika kipindi cha miezi mitatu ya awali ambapo kwa jiji la Tanga wameanza kutoa hati 110 na Muheza hati 131.

Baadhi ya wananchi waliyopatiwa vocha zao waliipongeza idara hiyo kwa kazi nzuri waliyoahidi kuwapatia na kuwezeshwa kupata hati zao kwa muda kwa kutumia huduma ya vituo jumuishi kwani imewapunguzia usumbufu pamoja na garama ya usafiri.

“Tunapongeza na kuushukuru uongozi wa Ardhi hapa mkoani kwa kuturahisishia huduma ya upatikanaji wa hati kwa kutumia huduma ya pamoja ya kituo jumuishi ambapo wote tuliolipa tumepata kwa wakati mmoja tena kwa muda mfupi” alisema Elisa Materu.

“Utaratibu huu walioanzisha unasaidia sana kupunguza garama tofauti na miaka iliyopita ilikuwa kuipata hati ni tatizo, lakini kwa sasa hakuna usumbufu ule, unakaa nyumbani tu unapogiwa simu kwamba hati yako tayari, kama kuna matatizo madogo madogo nina imani yataendelea kutatuliwa, hivyo niwaombe wananchi wenzangu wake kulipia wapate hati zao” alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!