Home Kitaifa WANANCHI WA KIBAHA KUNUFAIKA NA MIRADI MIKUBWA NA YA KIMKAKATI

WANANCHI WA KIBAHA KUNUFAIKA NA MIRADI MIKUBWA NA YA KIMKAKATI

Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Mhe. Sarah Msafiri amewatoa hofu wananchi wanaopitiwa na miradi mikubwa ya kimkakati wilayani humo kuwa hakuna atakayehamishwa bila kulipwa fidia.

Akizungumza katika mkutano wa Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji, Maofisa Tarafa na Madiwani Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Mhe. Sarah Msafiri amesema lengo la kutekelezwa kwa miradi hiyo mikubwa ni pamoja na kuwa ufaisha wananchi.

Amesema mkoa wa Pwani umependelewa maana miradi inayopangwa kutekelezwa ukiwemo wa Bandari Kavu ambao umefikia asilimia 75, Reli ya Kisasa Standard Gauge na Jiji la Kimataifa la Kisasa la Kwala haitekelezwi mahala pengine nchini.

Miradi hii ni mali yetu wananchi wa Kibaha, tunapaswa kujivunia na kuilinda na hakuna mtu ambaye atatakiwa kupisha baadhi ya maeneo ambaye hatalipwa fidia” DC Sarah Msafiri

Amesema kupitia miradi hiyo kutakuwa na fursa nyingi za kiuchumi na ajira wakati wa utekelezaji maana wenyeji ndiyo watapewa kipaumbele cha kwanza katika kuajiriwa.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kibaha Nuru Butamo amewataka Wananchi kuwa walinzi wa miradi hiyo mikubwa ambayo ipo kwa manufaa yao.

Naye msimamizi wa Ujenzi wa SGR kipande cha Dar – Morogoro Omary Paul akizungumza katika mkutano huo amesema ujenzi katika kipande anachokisimamia umefikia asilimia 97.

Amesema katika ujenzi wa kipande anachokisimamia sehemu kubwa ya reli ipo mkoani Pwani takribani Km 95 hivyo wanufaika wakubwa wa mradi huo ni wakazi wa Pwani kutokana na kuwepo kwa mahitaji makubwa ya bidhaa mbalimbali ikiwemo Sukari, Mahindi, Mchele na Mbogamboga.

Amesema ujenzi wa vivuko vya wananchi na mifugo umefanyika kwa makubaliano na wananchi na tayari fedha za fidia zimeshatolewa bado kuwafikishia walengwa na kila anaye stahili atalipwa.

Mkutano huo pia ulihudhuriwa na afisa habari wa Bonde la Wami Ruvu Bilali Sadat ambaye amesema ipo haja ya kuwa na matumizi bora ya maji kwa wakazi waliopo pembezoni mwa mto Ruvu.

Amesema watakuwa wakiwashirikisha wananchi katika mipango yote ya matumizi ya maji hasa ya shughuli za Kilimo ili kuulinda mto kwa kufanya kilimo cha kisasa.

Sadat ameeleza kuwepo kwa mpango wa kuangalia uwezekano wa kuwa na Kilimo cha michikichi ambapo kwa kushirikiana na watalaam wa Kilimo wanaangalia kama kilimo hicho hakitakuwa na athari kwa mto Ruvu.

mkutano huo wa Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji, Maofisa Tarafa na Madiwani uliisha kwa kukubaliana kwamba, kukamilika kwa miradi hiyo ukiwemo Jiji la Kisasa la kibiashara kutabadili taswira ya Wilaya ya Kibaha na kuinua uchumi wa wananchi wa wilaya hiyo na maeneo jirani.

Mwisho

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!