
Na Hamida Ramadhan,Mzawa Media Dodoma
WANAFUNZI wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) wanaosomea masomo ya Historia na Malikale wametakiwa kutoa elimu kwa jamii inayowazunguka katika kulinda na kuhifadhi urithi wa malikale na tamaduni za mtanzania ambayo itaongeza thamani kwa makabila na Taifa kwa ujumla.
Hayo yameelezwa jana Jijini hapa na
Mhadhiri Msaidizi Taaluma ya Urithi wa Utamaduni na Uendeshaji wa Makumbusho kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma, Selina Banzi wakati akizungumza katika Maonesho ya kabila la Wagogo yaliyoshirikikisha wanafunzi wanaosomea masomo ya Urithi wa Utamaduni, Historia na Utalii.
Maonesho hayo yalikuwa na lengo la kuwajengea uwezo, ufanisi na weledi wa kutoa elimu kwa jamii juu ya kulinda na kuhifadhi urithi wa watanzania.
Mhadhiri huyo msaidizi amesema elimu hiyo itasaidia jamii kujua mambo mbalimbali yanahohusu utamaduni wa mtanzania na hivyo kuongeza thamani ya makabila.

Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Sanaa na Taaluma za Habari Chuo Kikuu Dodoma, Dk Deograsia Ndunguru amesema “Lengo la fani hizi katika chuo hiki, ni kuzalisha wataalamu wabobezi watakao hudumu katika kuendeleza na kuhifadhi urithi wetu malikale na kiutamaduni na kutumia rasilimali hizo kama zao la kiutalii ili kushamirisha uchumi wa nchi yetu.
Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya mambo ya kale anayeshughulikia maendeleo ya Malikale na Makumbusho, Mwita William amesema Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Idara ya Malikale itaendelea kushirikiana na chuo kikuu cha Dodoma kwa kushirikiana na Idara ya Historia na Akiolojia ili kuongeza nguvu katika kulinda na kuhifadhi urithi wa Malikale, historia na tamaduni.
Naye, Chifu Mazengo mtawala wa kimila kutoka katika jamii ya wagogo ametoa wito kwa jamii kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhifadhi urithi wa watanzani hasa katika kipindi hiki cha utandawazi unaoingiza tamaduni nyingi za kigeni ndani ya nchi ikiwemo lugha, mavazi, vyakula na mwenendo wa maisha
Itakumbukwa kuwa miongoni mwa malengo matano ya sera ya utamaduni ya mwaka 1997 nchini Tanzania ni kushirikisha shughuli za Utamaduni wa Taifa kuanzia shule za awali, Sekondari na elimu ya Juu na kuhakikisha mafunzo ya hayo yanaingizwa katika mitaala na muhtasari na kufundishwa shuleni

Mwisho