
Na Shomari Binda-Musoma
MADAKTARI bingwa wa macho kutoka hospitali ya Kanda ya Bugando Mwanza wataweka kambi ya siku 5 mjini Musoma kwenye hospitali ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.
Akizungumza na Mzawa Blog Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo Dk.Osmundi Dyegura amesema huo ni muendelezo wa kuwasogezea huduma za kibingwa wananchi.
Amesema taratibu za kuwapokea madaktari hao na kuanza kutoa huduma kuanzia februari 10 hadi 14 zinaendelea vizuri.
Dk. Dyegura amesema wananchi wote wanaosumbuliwa na matatizo ya macho wanapaswa kujiandaa kukutana na madaktari ili waweze kuhudumiwa.
Amesema wananchi wanaotumia bima watahudumiwa na wasiokuwa na bima watahudumiwa kwa gharama za kila siku za hospitali.
Mganga Mfawidhi huyo amesema katika kipindi chote cha utoaji wa huduma kwa wote wenye shida ya macho madaktari hao kutoka Bugando watashirikiana na madaktari na wahudumu waliopo hospitali ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.
” Kuanzia jumatatu ya februari 10 tutakuwa na madaktari bingwa wa macho kutoka hospitali ya kanda Bugando kutoa huduma kwa siku 5 kwa wananchi.
” Wananchi wenye matatizo ya macho watumie fursa hii kufika hospitalini ili waweze kuhudumiwa na kuepuka gharama kubwa za kufuata huduma jijini Mwanza”,amesema.
Hospitali ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere imekuwa na utaratibu wa kushirikiana na madaktari bingwa kutoka hospitali ya rufaa ya kanda Bugando kutoa huduma ya magonjwa mbalimbali kwa wananchi.