
Mkuu wa Tawi la Operation na Mafunzo wa JKT, Brigedia Jenerali Peter Mnyani,akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 12,2026 katika Mako Makuu ya JKT Chamwino Mkoani Dodoma kuhusu wito wa kuripoti makambini vijana waliochaguliwa kujiunga na mafaunzo ya JKT kwa mujibu wa sheria 2026.
Na.Alex Sonna-CHAMWINOÂ
Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa JKT Meja Jenerali Rajab Mabele amewataka Vijana waliohitimu kidato cha Sita kwa Mwaka 2026, Tanzania Bara na Visiwani ambao wamechaguliwa kujiunga na Mafunzo ya JKT kwa Mujibu wa sheria ambao hawajaripoti kwenye kambi waliyopangiwa, kwenda kuripoti kwenye makambi yaliyokaribu nayo kuanzia juni 12 hadi Juni 15, 2026.
Akizungumza Wilayani Chamwino Mkaoni Dodoma kwa niaba ya Mkuu wa JKT, Mkuu wa Tawi la Operation na Mafunzo wa JKT, Brigedia Jenerali Peter Mnyani amesema awali Mkuu wa JKT Meja Jenerali Rajabu Mabele alitoa wito kwa vijana hao kuanza kuripoti kuanzia juni mosi hadi juni 7 ambapo baadhi ya vijana walishindwa kuripoti kwenye makambi waliyopangiwa kutokana na changamoto mbalimbali.
Amesema vijana hao wanatakiwa kuripoti kwenye kambi yoyote iliyokaribu nao, isipokuwa kambi ya Ruvu JKT iliyopo Mlandizi Mkoani Pwani, JKT Makutupora iliyopo Mkoani Dodoma na Chuo Cha uongozi Cha JKT (CUJKT) kilichopo Kimbiji Jijini Dar es salaam.
Ameongeza kuwa Mkuu wa JKT Meja Jenerali Rajabu Mabele anawakaribisha vijana wote waliohitimu kidato cha sita kwa mwaka 2026 ili waweze kujiunga na vijana wenzao katika kujengewa uzalendo, kufundishwa nidhamu, ukakamavu, umoja wa kitaifa, stadi za kazi, stadi za maisha na utayari wa kulijenga na kulitumikia taifa.
Katika hatua nyingine amebainisha kuwa kwa wahitimu wenye ulemavu wa kuonekana kwa macho wao wataripoti katika kambi ya Ruvu JKT iliyopo Mlandizi Mkoani Pwani ambayo ina miondombinu ya kuwahudumia watu hao.









