Home Kitaifa WAFUGAJI RUFIJI WAPATIWA HATI MILIKI, WAPONGEZA SERIKALI

WAFUGAJI RUFIJI WAPATIWA HATI MILIKI, WAPONGEZA SERIKALI

Na Julieth Mkireri, Rufiji

Wafugaji wilayani Rufiji wameishukuru Serikali ya Wilaya kwa kushirikiana na Chama cha Wafugaji kwa kujenga maeneo kwa ajili ya wafugaji kupitia mpango wa matumizi bora ya ardhi na kupatiwa hati miliki.

Zaidi ya wafugaji 50 wamepatiwa hati miliki hizo, hali itakayopunguza migogoro ya mara kwa mara kati ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi.

Ugawaji wa hati miliki hizo umefanywa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Wazo Mwang’onda, jana Aprili 26, 2026 katika kata ya Chumbi baada ya Mwenge kutembelea eneo maalumu kwa ajili ya wafugaji.

Pongezi za wafugaji hao zimetolewa na Lisesi Tunung’u, ambaye alisema awali maisha yao yalikuwa ya kuhama-hama na kwa sasa wanamiliki ardhi yao kwa ajili ya kuendesha shughuli za ufugaji.

Kwa upande wake, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Wazo Mwang’onda, ameipongeza Halmashauri ya Mji Rufiji kwa kutekeleza mpango wa ranchi ndogo na kupunguza migogoro.

Nawapongeza Wilaya ya Rufiji kwa kazi hii nzuri na wawekezaji wetu ambao wamewekeza katika ufugaji kwa sababu hii ni biashara. Mwenge wa Uhuru umeridhishwa na utekelezaji wa ranchi hizi,” amesema Mwang’onda.

Awali, akisoma taarifa ya utekelezaji wa ranchi hizo, Mkuu wa Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Halmashauri ya Mji Rufiji, Ryoba Magabe, alisema Wilaya ya Rufiji inatekeleza mpango wa ranchi ndogo kwa ajili ya kuwapanga wafugaji.

Amesema wafugaji watapangwa kwenye vitalu maalumu vya ufugaji vyenye ukubwa wa hekari 125, ambapo kwa kata ya Chumbi kuna vitalu 58.

Mwenge wa Uhuru umekagua na kuweka jiwe la msingi miradi saba yenye thamani ya shilingi bilioni 4.95.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!