
WAZIRI wa Kazi na Uwekezaji Zanzibar, Shariff Ali Shariff, amewataka Watanzania, wafanyabiashara na wadau wa maendeleo kushiriki kikamilifu katika Tamasha la pili la Uwekezaji Zanzibar litakalofanyika kuanzia Juni 3 hadi 5 mwaka 2026 katika ukumbi wa Golden Tulip Airport Zanzibar.
Pia amesema Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, anatarajiwa kuwa mgeni katika Tamasha la pili la Uwekezaji Zanzibar mwaka 2026.

Hayo yalisemwa leo Aprili 27, 2026 jijini Dar es Salaam, ambapo Waziri Shariff amesema kongamano hilo litawakutanisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, watunga sera, wafanyabiashara wakubwa pamoja na wadau wa maendeleo kutoka sekta mbalimbali kwa lengo la kujadili na kuonesha fursa za uwekezaji zilizopo Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Amesema tamasha hilo ni jukwaa muhimu kwa Watanzania na litawanufaisha kwa kutoa fursa za uwekezaji zilizopo nchini, hivyo ushiriki wao utachangia kukuza uchumi wa taifa kupitia ongezeko la ajira, mapato ya serikali na kuboresha maisha.

“Tunapenda kutoa wito kwa Watanzania wote, wawekezaji, wafanyabiashara, taasisi za fedha, washirika wa maendeleo, wanadiaspora na wadau wote kushiriki kikamilifu katika tukio hili muhimu,” amesema.
Aidha, amesema washiriki wa kongamano hilo watapata fursa ya kutembelea miradi mbalimbali ya uwekezaji, ikiwemo hoteli za kisasa, miradi ya utalii wa baharini, viwanda pamoja na maeneo maalum ya uwekezaji (industrial parks).
Vilevile, amesema kutakuwa na maonyesho ya biashara, majadiliano ya kitaalamu, madarasa maalum na mikutano ya ana kwa ana kati ya wafanyabiashara.
“Kaulimbiu ya tamasha hilo inalenga ‘Promoting Investment Diversification for Sustainable Development in Zanzibar, Shaping Zanzibar’s Next Growth Story,’ huku serikali ikiwa imeandaa miradi ya kimkakati itakayowezesha sekta binafsi kushirikiana na serikali katika kukuza uchumi na kuongeza ajira nchini.”

Naye Mkurugenzi wa Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), Saleh Saad Mohamed, amesema Zanzibar imeendelea kushuhudia ongezeko la miradi ya uwekezaji yenye thamani kubwa, hatua inayochangia ukuaji wa uchumi na kuongeza ajira.
Amesema mafanikio hayo yanatokana na juhudi za serikali za kuboresha mazingira ya biashara na kuvutia wawekezaji, huku baadhi ya miradi ikielekezwa katika sekta muhimu kama utalii, miundombinu na uchumi wa buluu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TISEZA, Gilead Teri, amesema ushirikiano kati ya taasisi za uwekezaji za Tanzania Bara na Zanzibar umeimarika, hivyo umekuwa na matokeo chanya katika kuvutia uwekezaji.
Hata hivyo, amesema taasisi hizo zinaendelea kushirikiana kutangaza fursa za uwekezaji ndani na nje ya nchi na kusisitiza umuhimu wa kuongeza ushiriki wa wawekezaji wazawa ili kuhakikisha manufaa ya uwekezaji yanawanufaisha Watanzania kwa ujumla.
Tamasha hilo linatarajia kuleta zaidi ya washiriki 500 kutoka ndani na nje ya nchi, wakiwemo wawekezaji wa kitaifa na kimataifa, watunga sera, wafanyabiashara wakubwa, washirika wa maendeleo pamoja na wanadiaspora, huku tamasha likilenga kupanua wigo wa uwekezaji Zanzibar na Tanzania kwa ujumla katika sekta ya uchumi wa buluu, afya na usafiri wa anga.









