
Kariakoo, 31 Julai, 2026
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Kikodi Kariakoo imeendelea kuimarisha ushirikiano na walipakodi kupitia mikutano ya ana kwa ana (Outreach) inayolenga kusikiliza, kutatua changamoto na kutoa elimu ya kodi ili kuwawezesha walipakodi kutekeleza wajibu wao kwa hiari.
Ziara hiyo ilifanyika katika eneo la Raha Square, Kariakoo, ambapo maafisa wa TRA walisikiliza maoni ya wafanyabiashara, wakatoa ufafanuzi wa masuala ya kodi na kutatua baadhi ya changamoto zilizowasilishwa.
Kufuatia mazungumzo hayo, Kiongozi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo Bw. Severine Mushi alieleza kuwa dhamira yao ya kuendelea kushirikiana na TRA kwa kutimiza wajibu wao wa kulipa kodi kwa hiari.
“Tunawashukuru TRA kwa kututembelea na kuwa na Utaratibu huu wa kutufikia katika maeneo yetu ya biashara kwani umewezesha kueleza changamoto kwa uwazi, kupata ufafanuzi wa masuala ya kodi na kujenga uelewa unaotuongezea imani na kuhamasishana kutekeleza wajibu wa kikodi kwa hiari.” Alisema Mushi
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa TRA -Kariakoo, Edson Issanya, aliwahimiza wafanyabiashara wenye changamoto zinazohusiana na masuala ya kodi kufika katika ofisi za TRA ili zipatiwe ufumbuzi kwa wakati.
Alisisitiza kuwa TRA itaendelea kuwa karibu na walipakodi kwa kutoa huduma bora, kusikiliza maoni yao na kuweka mazingira rafiki yatakayorahisisha utekelezaji wa majukumu ya kikodi na kuimarisha ushirikiano kati ya mamlaka na walipakodi.









