Wachezaji wa Klabu ya Simba Sc hii leo wakiwa katika maandalizi ya mwisho kuelekea tamasha kubwa la SIMBA DAY ambapo inatarajiwa kucheza dhidi ya Mabingwa wa soka ligi kuu ya Ethiopia klabu ya St. George Sc wametumia muda wao kuhamasisha wananchi kujitokeza katika zoezi la Sensa la Agosti 23.
Wachezaji hao wakiongozwa na Kapteni John Bocco, wameungana na Shomari Kapombe, Aishi Manula, Erasto Nyoni na wazawa wengine kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan kuwa wako tayari kuhesabiwa.
“Sisi wachezaji wa Simba Sc tunapenda kuwahamasisha watanzania wajitokeze kuhesabiwa kwani ni muhimu kwa maendeleo na mipango ya nchi yetu, tumuunge mkono Rais Samia katika zoezi hili”- Anasema Shomari Kapombe Beki wa kulia wa Simba.
Naye Clatous Chama amewaasa watanzania kujitokeza kuhesabiwa kwani zoezi hilo hufanyika nchi zote ili kuweka utaratibu mzuri wa maendeleo ya nchi.
Chama anaungana na wachezaji wengine wa kigeni ikiwemo Joash Onyango pamoja na Victor Akpan kuwaasa watanzania kujitokeza kuhesabiwa tarehe 23 Agosti, 2022.