
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) linaendelea kuimarisha ushirikiano na jamii kwa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kulinda na kuhakikisha usalama wa miundombinu ya bomba la gesi asilia katika vijiji vya Mkwalia Kitumbo na Sunguvuni, wilayani Mkuranga mkoani Pwani.
Akizungumza wakati wa utoaji wa elimu hiyo, Afisa Mwandamizi wa Maendeleo ya Jamii wa TPDC, Bw. Oscar Mwakasege amesema programu hiyo ni sehemu ya mkakati wa shirika wa kushirikisha jamii katika kulinda miundombinu ya gesi asilia katika kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu matumizi salama ya maeneo yanayopitiwa na bomba la gesi asilia pamoja na kuwajengea uwezo wa kutambua viashiria vinavyoweza kuhatarisha usalama wa miundombinu hiyo muhimu ya taifa.
“Lengo letu ni kuhakikisha wananchi wanaelewa umuhimu wa bomba la gesi asilia, namna ya kulilinda na kutoa taarifa mapema wanapoona viashiria vya uharibifu au shughuli zisizo salama karibu na miundombinu hiyo,” alisema Bw. Mwakasege.
Wananchi walioshiriki katika mikutano hiyo wameipongeza TPDC kwa kuwafikia moja kwa moja vijijini na kutoa elimu inayosaidia kulinda rasilimali za taifa huku ikijenga uelewa wa pamoja kuhusu masuala ya usalama.
Zoezi la utoaji wa elimu kwa Umma litaendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Pwani ikiwa ni sehemu ya juhudi za TPDC za kuimarisha usalama wa miundombinu ya gesi asilia na kujenga mahusiano mazuri kati ya shirika hilo na jamii inayozunguka mradi wa gesi asilia.






