
WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dk Juma Homera amesema watu wanaoitukana Serikali, kufanya uchochezi na vitendo visivyo vya maadili mitandaoni, majina yao yameshakabidhiwa kwa Wizara ya Mambo ya Ndani ili Jeshi la Polisi ili wachukuliwe hatua za kisheria.
Aliyasema hayo jana wakati akifungua mkutano wa siku wa mafunzo kwa mawakili wa serikali yaliyoandaliwa na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali jijini Arusha.
Dk. Homera alitoa kauli hiyo akijibu ombi la Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Dk. Damas Ndumbaro aliyetaka mawakili wa serikali kuisaidia Serikali dhidi mashambulizi na upotoshaji unaofanywa mitandaoni.
Dk. Homera alisema majina ya wahusika wa uhalifu huo tayari yamekabidhiwa Wizara ya Mambo ya Ndani kwa hatua za kisheria.
Alisema kuna Sheria ya Mitandao, sheria za Jeshi la Polisi na sheria ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ambazo zinadhibiti upotoshaji, uchochezi na uvunjifu wa maadili, hivyo serikali itahakikisha inazisimamia ili kukomesha uhali huo nchini.
“Serikali haikatai kukosolewa, lakini ikoselewa kwa jambo la haki na kweli na si jambo la uongo, na kutumia lugha ya matusi au uchochezi, hivyo wahusika watachukuliwa hatua za kisheria ili kuimarisha amani na usalama,”alisisitiza Dk Homera.
Aliongeza”Jeshi la Polisi limeanza kuchukua hatua dhidi ya wanaoitukana serikali, kufanya uchochezi na vitendo visivyo vya maadili mitandaoni.”
Kuhusu mafunzo hayo, alisema yatawasaidia mawakili wa serikali kuishauri serikali ipasavyo na kwa weledi, kuwa na uelewa mpana wa masuala mbalimbali, kujengewa uelewa kuhusu miradi ya ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP) na masuala mengine mbalimbali.
Alisema Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali inafanya kazi nzuri ya kuitetea serikali katika mashauri mbalimbali na kufanikiwa kuisadia serikali kuokoa zaidi ya shilingi trilioni moja kwa kushinda kesi hizo.
Naye Wakili Mkuu wa Serikali, Dk Ally Possi alisema katika kipindi cha Julai 2025 hadi Machi 2026, kati ya mashauri 641, serikali ilishinda mashauri 595 sawa na asilimia 88.1 na kuokoa Sh bilioni 316.3 ambayo serikali ingelipa kama ingeshindwa mashauri hayo.
Kuhusu mashauri ya usuluhishi, alisema mashauri 18 yamekamilika na serikali kuokoa Sh bilioni 6.8 katika kipindi hicho.
“Kwa hiyo katika mashauri yote ya madai na usuluhishi kuanziaJulai 2025 hadi Aprili 2026, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali tumeisadia Serikali kuokoa shilingi trilioni 1.35,”alisema Dk Possi.
Aliongeza”Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ilianzishwa mwaka 2018, na moja ya mafanikio makubwa tuliyoyapata ni kuitetea serikali katika kesi ya kukamatwa kwa ndege yetu na kushinda.”
Pia alisema mafunzo hayo kwa mawakili wa serikali yanalenga kulinda kila senti ya mlipakodi, kutetea rasilimali za serikali, kuongeza uwezo wa mawakili katika nyanja mbalimbali, kujinoa kitaaluma, na kuendesha mashauri kwa weledi na umahiri.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Dk. Damas Ndumbaro alisema kuna haja kwa mawakili wa serikali kuja na mpango wa namna ya kuitetea serikali dhidi ya mashambulizi na upotoshaji mkubwa dhidi ya serikali.
“Nini nafasi ya mawakili wa Serikali katika jambo hili? Nashauri kupitia mafunzo haya jadilianeni nini cha kufanya ili kuihudumia nchi na jamii yetu kwa weledi,”alisema Dk. Ndumbaro
Pia alisema kwa kuwa asilimia 36 ya migogoro yote iliyoibuliwa na timu ya Msaada wa Kisheria ya Samia imetokana na ardhi, hivyo alimuomba Wizara ya Katiba na Sheria kulifanyia utafiti jambo hilo ili kujua chanzo na kuja na suluhu ya kuikomesha migogoro hiyo.
Dk Ndumbaro aliwataka mawakili hao wa serikali kujifunza kwa vitendo kupitia mashauri mbalimbali wanayoshinda na kushindwa ili kufanya mabadiliko ya kisheria yanayohitajika kwa maslshi ya taifa na kuleta ufanisi katika sekta ya sheria.
Kwa mujibu wake, Februari 2018, Tanzania ilifanya mageuzi makubwa katika sekta ya sheria nchini kwa kupangilia upya nafasi tatu ikiwemo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP).
Alisema mageuzi hayo yamesaidia kuleta ufanisi katika sekta ya sheria nchini.
Naye Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Alice Mtulo alisema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo Mawakili wa serikali kuhusu uendedhaji wa mashauri ya madai na usuluhishi.
Alisema jumla ya washiriki 600 wanahudhuria mafunzo hayo wakiwemo mawakili kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, taasisi za serikali na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali.
Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Samwel Maneno alisema mawakili wa serikali wanawajibu wa kuisaidia serikali kwa kutoa ushauri mzuri wa kisheria pale serikali inapoingia mikataba na sekta binafsi ambayo ni injini ya uchumi wa taifa.
Maneno alisema Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeshasajili mawakili zaidi ya 30 katika kitengo cha ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP) katika kutekeleza miradi ya ubia.
Naye Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Zanzibar, Shaaban Abdalla aliwataka mawakili hao wa serikali kusimamia mashauri ya madai na usuluhishi kwa weledi na uzalendo kupitia mafunzo wanayopewa.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama Tanzania, Profesa Elisante Ole Gabriel alisema kwa kuwa Mahakama ni chombo cha juu na cha mwisho katika kutoa haki, hivyo Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ni mdau muhimu katika jambo hilo.









