Home Kitaifa KIONGOZI WA MBIO ZA MWENGE WA UHURU 2026 AIPONGEZA REA KWA UHAMASISHAJI...

KIONGOZI WA MBIO ZA MWENGE WA UHURU 2026 AIPONGEZA REA KWA UHAMASISHAJI WA NISHATI SAFI YA KUPIKIA

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2026, Ndugu Wazo Michael Mwang’onda, ameipongeza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa juhudi kubwa inazoendelea kuzifanya katika utekelezaji wa miradi ya nishati safi ya kupikia nchini, akieleza kuwa miradi hiyo imekuwa na mchango mkubwa katika kuhamasisha wananchi kutumia nishati safi, salama na rafiki kwa mazingira.

Pongezi hizo amezitoa wakati alipotembelea banda la REA katika maonesho yanayoendelea sambamba na Mbio za Mwenge wa Uhuru katika Halmashauri ya Wilaya ya Madaba mkoani Ruvuma, ambapo alipata fursa ya kujionea shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na wakala huo katika kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata huduma ya nishati safi ya kupikia kwa gharama nafuu.

Akizungumza mara baada ya kutembelea banda hilo, kiongozi huyo amesema REA imeendelea kuwa chachu muhimu katika utekelezaji wa ajenda ya taifa ya matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kuendelea kutoa elimu kwa wananchi pamoja na kuweka mazingira wezeshi ya upatikanaji wa vifaa vya nishati safi kwa bei nafuu.

Amesema matumizi ya nishati safi ya kupikia yana manufaa makubwa kwa wananchi kwani yanasaidia kupunguza madhara ya kiafya yanayotokana na moshi wa kuni na mkaa, huku pia yakichangia utunzaji wa mazingira kwa kupunguza ukataji wa miti na uharibifu wa misitu.

Tunapaswa kuendelea kuunga mkono juhudi hizi zinazofanywa na REA kwa sababu nishati safi ya kupikia siyo tu inalinda mazingira, bali pia inaleta nafuu kwa wananchi na kuboresha afya za familia nyingi,” amesema.

Aidha, ametoa wito kwa REA kuendelea kusimamia na kutekeleza miradi hiyo kwa bidii zaidi ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi, hususan wa maeneo ya vijijini na wenye kipato cha chini, wanapata fursa ya kutumia nishati safi ya kupikia.

Katika hatua nyingine, kiongozi huyo amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kutumia fursa zinazotolewa kupitia miradi hiyo ya ruzuku ili waweze kuachana na matumizi ya nishati zisizo rafiki kwa mazingira na afya.

Akiwasilisha taarifa kuhusu shughuli zinazotekelezwa na REA, Mhandisi wa Miradi kutoka REA, Davidi Malima, amesema wakala huo unaendelea kutekeleza mradi wa usambazaji na uuzaji wa mitungi ya gesi ya kilo sita kwa bei ya ruzuku kwa wananchi katika maeneo mbalimbali nchini.

Amesema kupitia mradi huo, wananchi wanapata fursa ya kununua mitungi ya gesi kwa gharama nafuu zaidi ikilinganishwa na bei ya kawaida ya soko, hatua inayolenga kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia katika jamii.

“Mitungi hii ambayo kwa kawaida huuzwa kwa takribani shilingi elfu hamsini, sasa inapatikana kwa bei ya ruzuku ya shilingi elfu kumi na tisa na mia tano tu. Mwananchi atatakiwa kuwa na Kitambulisho cha Taifa (NIDA) ili kupata mtungi huo,” amesema Mhandisi Malima.

Ameongeza kuwa REA imeendelea kutoa ruzuku pia kwa majiko banifu ambayo yamekuwa yakisaidia kupunguza matumizi makubwa ya kuni na mkaa, huku yakichochea matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa wananchi wengi zaidi.

Kwa mujibu wa Mhandisi Malima, lengo kuu la utoaji wa ruzuku hiyo ni kuwafikia wananchi wa kipato cha chini na kuwawezesha kumudu gharama za vifaa vya nishati safi ya kupikia, sambamba na kuongeza uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa matumizi ya nishati hiyo.

Amesema REA itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha ajenda ya taifa ya matumizi ya nishati safi ya kupikia inafanikiwa na kuwafikia wananchi wengi zaidi nchini.

Mwisho.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!