Home Biashara TIGO PESA WATOA ZAIDI YA MILIONI 300 KWA MAWAKALA WAKE NCHI NZIMA

TIGO PESA WATOA ZAIDI YA MILIONI 300 KWA MAWAKALA WAKE NCHI NZIMA

Na Mwandishi Wetu.

Dar es Salaam 16 Novemba 2023: Mawakala wa Kampuni ya mtandao wa simu za mkononi wa Tigo wanaotoa huduma za miamala maarufu kama Tigo Pesa leo imekuwa siku yao ya furaha kufuatia kampuni hiyo kutoa zaidi ya milioni 300 kwa mawakala hao nchi nzima.

Mkuu wa Usambazaji Huduma wa Tigo Pesa, Innocent Mosha akimkabidhi mfano wa Hundi mmoja wa mawakala washindi  aliyejitambulisha kwa jina la Twisile Hilliard.

Mkuu wa Usambazaji Huduma wa Tigo Pesa, Innocent Mosha akiwa na baadhi ya mawakala baada ya kuwakabidhi maokoto yao.

Akizungumza kwenye hafla ya kuwakabidhi maokoto yao baadhi ya mawakala waliopo jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Usambazaji Huduma wa Tigo Pesa, Innocent Mosha alisema;

“Naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutukutanisha hapa leo, Nichukue nafasi hii kuwakaribisha wote katika hafla hii ya utoaji wa hundi mfano kwa washindi wa promosheni yetu ya Mawakala wa Tigo Pesa. “Promosheni hii ya Tigo Pesa Wakala Push, ilianzishwa ili kuwapa motisha mawakala wetu katika kutekeleza majukumu yao na pia kuwashukuru kwa kujitoa kikamilifu kupambania malengo ya kibiashara tuliyokubaliana kwa pamoja.

“Leo, tunatoa zaidi kwa mawakala 33 nchi nzima walioibuka washindi katika promosheni hii. Promosheni hii imeendeshwa kwa mwezi mzima wa Oktoba na leo tunawatunuku wale walioweza kufikia malengo yao ya biashara kwa kuwahudumia wateja wetu katika maeneo yao kwa ufanisi mkubwa. “Hii ni siku ya kipekee tunayoweza kusherehekea mafanikio ya mawakala wa Tigo Pesa kutoka maeneo mbalimbali, kama vile Mwanza, Zanzibar, Dar es Salaam, Arusha na Mbeya ambapo kwa ujumla mpaka leo tutakuwa tumetoa zaidi ya milioni 300m/- kwa mawakala walioibuka washindi. “Tunapoongelea juu ya mafanikio haya, ni muhimu kutambua wigo mpana wa huduma za Tigo Pesa. Tigo Pesa inatoa huduma kamili za kifedha kwa zaidi ya wateja milioni 13, na ili kutoa huduma zetu kwa ufanisi, lazima tuwawezeshe washirika wetu muhimu wa biashara, ikiwa ni pamoja na Tigo Pesa Wakala wanaochangia kiasi kikubwa kufikisha huduma za kifedha za Tigo Pesa kwa watanzania wote. “Tigo Pesa inajivunia wafanyabiashara 300,000 wanaotoa huduma za Lipa kwa Simu na takriban wakala wa Tigo Pesa 200,000 nchi nzima, vile vile Tigo Pesa tunaendelea kuwaletea wateja huduma za kibunifu zinazochangia ukuaji uchumi wa kidigitali hapa Tanzania kama vile Bustisha, Tigo Pesa Rafiki, Kibubu, Nivushe Plus, Tigo Kilimo, Bima Mkononi na nyingine nyingi.

“Nichukue fursa hii, kuwashukuru na kuwapongeza sana mawakala wetu wote kwa kazi kubwa na nzuri ya kutoa huduma bora kwa wateja wetu ili kukidhi mahitaji yao ya miamala ya kidigitali. Tunawashukuru wateja wetu kwa kuendelea kutumia huduma za Tigo Pesa. Tigo Pesa Zaidi Pesa!” Ahsanteni kwa Kunisikiliza”. Alimaliza kusema Innocent na kuanza kuwakabidhi mawakala hao maokoto yao.

Previous articleMWENYEKITI WA BODI YA NISHATI VIJIJINI AAGIZA MIRADI YOTE IKAMILIKE KABLA YA DESEMBA 2023
Next articleELIMU YA FEDHA KUFUNGUA FURSA ZA UKUAJI WA UCHUMI

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here