Na.Alex Sonna-DODOMA
OFISI ya Taifa ya Takwimu (NBS) imesema takwimu rasmi zitaendelea kuwa nguzo muhimu katika kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kuifanya Tanzania kufikia uchumi wa dola trilioni moja na kuongeza ustawi pamoja na kipato cha wananchi.
Kauli hiyo imetolewa leo Juni 17,2026b na Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi wa NBS, Daniel Masolwa, wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika viwanja vya Chinangali jijini Dodoma, ambapo taasisi hiyo inatoa elimu kwa wananchi kuhusu huduma zake na umuhimu wa takwimu katika maendeleo ya taifa.
Masolwa amesema kaulimbiu ya mwaka huu inayosema “Kuchochea Uwajibikaji Jumuishi kwa Huduma Endelevu” imeipa NBS fursa ya kueleza nafasi ya takwimu rasmi katika kupanga maendeleo, kufanya maamuzi sahihi na kufuatilia utekelezaji wa mipango mbalimbali ya kitaifa.
Amesema kwa mujibu wa Sheria ya Takwimu, Sura ya 351, NBS imepewa jukumu la kukusanya, kuchakata, kuchambua na kusambaza takwimu rasmi zinazotumika katika sekta mbalimbali za maendeleo nchini.
“Takwimu rasmi ni msingi wa upangaji wa maendeleo. Serikali, sekta binafsi, watafiti na wadau wengine hutegemea takwimu hizi katika kufanya maamuzi sahihi na kupima matokeo ya mipango inayotekelezwa,” amesema Masolwa.
Amebainisha kuwa miongoni mwa takwimu zinazozalishwa na NBS ni zile za mfumuko wa bei zinazotolewa kila mwezi na kuonesha mwenendo wa bei za bidhaa na huduma nchini.
Aidha, amesema ofisi hiyo huzalisha takwimu za Pato la Taifa (GDP) kwa vipindi vya robo mwaka, ambazo huonesha thamani ya bidhaa na huduma zinazozalishwa nchini, kasi ya ukuaji wa uchumi pamoja na mchango wa sekta mbalimbali katika maendeleo ya uchumi wa taifa.
Masolwa ameongeza kuwa NBS pia huzalisha takwimu za ajira zinazoonesha hali ya soko la ajira, kiwango cha ukosefu wa ajira, idadi ya watu waliopo katika ajira na wale waliopo nje ya nguvu kazi.
“Tunaendelea kuzalisha takwimu za kilimo, uzalishaji viwandani, biashara ya nje pamoja na takwimu za kijamii zinazotokana na Sensa ya Watu na Makazi, ambazo zinaonesha mwenendo wa idadi ya watu, mgawanyo wa umri na rasilimali watu iliyopo nchini,” amesema
Amefafanua kuwa takwimu hizo ni nyenzo muhimu katika kupima viashiria mbalimbali vya maendeleo, ikiwemo wastani wa pato la mwananchi, kiwango cha ukuaji wa uchumi na hali ya maisha ya wananchi kwa ujumla.
Akizungumzia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Masolwa amesema mafanikio ya utekelezaji wake yatategemea kwa kiwango kikubwa uwezo wa nchi kutumia takwimu katika kupanga, kufuatilia na kutathmini hatua zinazopigwa kuelekea malengo yaliyowekwa.
“Lengo la Dira 2050 ni kuwa na uchumi mkubwa, shindani na unaotoa ustawi kwa wananchi ili kufikia azma hiyo, tunahitaji jamii inayojifunza, inayozalisha maarifa, inayotumia ujuzi na inayofanya maamuzi kwa kuzingatia takwimu sahihi na za kuaminika,” amesema
Amesisitiza kuwa NBS itaendelea kuhakikisha takwimu rasmi zinapatikana kwa wakati, kwa ubora unaohitajika na kwa viwango vya kimataifa ili kusaidia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na juhudi za kuharakisha maendeleo ya Tanzania.












