
Tanzania ina utajiri wa rasilimali za madini ya chuma, vanadiamu na titaniamu, ambayo yatachimbwa na kusindikwa hapa nchini ili kutosheleza mahitaji ya soko la ndani na nje ya Nchi.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Balozi Waziri Salum, Machi 30, 2026, jijini Dodoma wakati wa kikao na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Fangda Group kutoka nchini China
Bw. Ao Xinhua na ujumbe wake.Kikao hicho kililenga kutathmini fursa za uwekezaji katika sekta ya viwanda na biashara, hatua inayokusudia kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uzalishaji viwandani na uongezaji thamani wa rasilimali barani Afrika.

Aidha, Amesisitiza kuwa lengo si kusafirisha malighafi pekee, bali ni kuanzisha viwanda vya bidhaa za mwisho ili kuzalisha ajira kwa wazawa, kukuza ujuzi wa kiteknolojia na kuokoa fedha za kigeni zinazotumika kuagiza bidhaa hizo kutoka nje ya nchi.
Balozi Salum pia amebainisha kuwa Tanzania imejipambanua kama lango kuu la soko lenye zaidi ya watu milioni 300 katika jumuiya za EAC na SADC kupitia miundombinu ya Reli ya Kisasa (SGR) na Bandari ya Dar es Salaam, inayorahisisha usafirishaji wa bidhaa kwenda nchi jirani zisizo na bandari.
Balozi Salum amewahimiza wawekezaji hao kutembelea maeneo ya uwekezaji huku akiahidi kuwa Serikali inaendelea kuweka mazingira bora ya uwekezaji na ufanyaji biashara ikiwemo vivutio vya kodi na urahisishaji wa taratibu ili kuwezesha miradi hiyo kwa manufaa ya pande zote mbili.
Kwa upande wa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Fangda Group kutoka nchini China Bw. Ao Xinhua amesisitiza dhamira yake ya kujenga uwezo wa uzalishaji ndani ya Afrika, uongezaji thamani wa rasilimali, usafiri wa anga na biashara. Hatua hiyo ni sehemu ya kuitikia mahitaji yanayoongezeka na kusaidia mapinduzi ya viwanda yatakayochochea maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi barani kote.








