NA.MWADISHI WETU
Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu Idara ya Menejimeti ya Maafa imeeleza itaendelea kuimarisha ushirikiano na wadau wa masuala ya maafa nchini ili kuendelea kusimamia na kuratibu masuala ya maafa nchini ili kuedelea kupunguza madhara yatokanano na maafa.
Akiwasilisha hotuba kwa niaba ya mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa wakati wa mkutano wa wadau wa masuala ya Afya Moja uliofanyika katika Ukumbi wa Edema Mkoani Morogoro Bi.Valentina Sanga alisema lengo la Serikali ni kuhakikisha masuala ya maafa yanaratibiwa na kusimamiwa kwa ufanisi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.
Mkutano huo ulihusisha wawakilishi kutoka katika wizara mbalimbali za kisekta, Ofisi ya Makamu wa Rais, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Afya, Wizara ya Kilimo, wawakilishi kutoka katika Taasisi mbalimbali za Umma ikiwemo;TAWIRI na TANAPA, na Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu NIMR, Waratibu wa Dawati la Afya Moja pamoja na washiriki kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Alieleza kuwa, kutokana na matukio ya hivi karibuni ya milipuko ya magonjwa kama vile janga la UVIKO – 19 ambalo limeathiri Nchi mbalimbali duniani; yamedhihirisha umuhimu wa kuimarisha ushirikiano katika kupambana nayo. Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua na inaendelea kuimarisha mashirikiano ya Kikanda na Kimataifa ikiwemo katika eneo la kupambana na changamoto za majanga yanayovuka mipaka na kuathiri sekta nyingi za kiuchumi na kijamii.
“Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais itaendelea kuimarisha ushirikiano huu katika eneo la uratibu na usimamizi wa maafa na magonjwa ya milipuko ikiwa ni pamoja na hatari nyingine za afya kama Usugu wa vimelea vya magonjwa kwa kuzingatia dhana ya Afya Moja,”alisema Valetina.
Akieleza kuhusu dhana ya Dhana ya Afya Moja Valentina alisema ni nyenzo muhimu ya kiutendaji inayozingatia ushirikiano katika kuandaa na kutekeleza mikakati ya pamoja ya kuzuia na kudhibiti magonjwa yanayoathiri afya ya binadamu, wanyama na mimea ili kutumia kwa ufanisi rasilimali chache zilizopo.
“Hatua hii ni muhimu katika kupambana na ongezeko la vimelea vya magonjwa ya kuambukiza kutoka kwa wanyama kwenda binadamu. Hali ambayo kwa kiasi kikubwa inachangiwa na mabadiliko ya tabianchi na athari katika mazingira zinazosababishwa na shughuli za kibinadamu zinazotekelezwa bila kuzingatia uhifadhi wa bionuai ikiwa ni pamoja na kilimo, ongezeko la watu, ukuaji wa miji na uvamizi wa binadamu katika makazi ya wanyamapori,”alisisitizaValetina.
Wakichangia hoja kwa wakati tofauti wajumbe kutoka Wizara ya Afya na Wizara ya Mifugo na Uvuvi waliahidi kuendelea kutoa ushirikiano pale unapohitajika na kuendelea kutekeleza maelekezo yote yanayotolewa ili kuhakikisha masuala haya yanatekelezwa kwa ufasini na mikakati ya pamoja katika kudhibiti magonjwa upande wa binadamu na wanyama kwa faida ya wananchi wote.
Naye Mwakilishi kutoka Shirika la Chakula Duniani FAO Dkt. Elibariki Mwakapeje alisema wataendelea kushirikiana na Serikali ili kuyafikia malengo yaliyopo.
“Mkutano huu ni muhimu ikiwa ni sehemu ya mchakato wa kutekeleza masuala ya Afya Moja, FAO tunatekeleza Sustainable development goals ambapo tunahakikisha hatuachi nyuma kundi lolote ikiwemo wenye ulemavu, hivyo tunaamini tutaendelea kutekeleza kupitia mfumo wa Four betters ikiwemo; better environment, better production, better nutrition and better life ili kuwa jamii salama,” alisisitiza Dkt. Mwakapeje
=MWISHO=