
Mgombea ubunge wa Jimbo la Kisarawe kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Selemani Jafo, amesema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita wamefanikiwa kufungua barabara kwa ajili ya kuchochea huduma za kiuchumi, ikiwemo mradi wa ujenzi wa barabara ya lami yenye urefu wa kilomita 34.5 ambayo kwa sasa ipo katika hatua ya ujenzi baada ya kupatikana mkandarasi.
Akizungumza leo, Septemba 9, 2025, katika kijiji cha Titu, kata ya Marui Marui, Jafo alisema endapo atapewa ridhaa kwa kipindi kingine, atahakikisha vitongoji vyote vilivyobakia ndani ya kata hiyo vinapata huduma ya umeme ndani ya siku 100.
Kuhusu sekta ya elimu, Jafo alikumbusha kuwa katika kipindi kilichopita aliahidi kujenga shule, na sasa kata hiyo tayari imepata shule mpya, jambo lililowaondolea wanafunzi adha ya kusoma katika kata nyingine. Amesema dhamira yake kwa miaka mitano ijayo ni kuhakikisha kata hiyo inapata shule nyingine ya sekondari.
Aidha, alisema Wilaya ya Kisarawe sasa ina sekondari sita za kidato cha tano na sita, pamoja na sekondari nane mpya. Alibainisha kuwa hakuna kata hata moja isiyo na shule ya sekondari, na juhudi zinaendelea kuhakikisha kila kata inaongezewa shule.








