Home Kitaifa KAMATI ITUSHAURI UWEKEZAJI WENYE TIJA KATIKA KIWANDA CHA GENERAL TYRE – BALOZI...

KAMATI ITUSHAURI UWEKEZAJI WENYE TIJA KATIKA KIWANDA CHA GENERAL TYRE – BALOZI SALUM

Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Mhe. Balozi Waziri Salum, ameiagiza kamati ya wataalamu kufanya uchambuzi na kutoa ushauri kuhusu uendelezaji wa eneo la Kiwanda cha kutengeneza matairi cha General Tyre, kilichosimamisha uzalishaji tangu mwaka 2007, kilichopo Mkoa wa Arusha.

Ameitaka kamati hiyo kupendekeza namna bora ya kulitumia eneo hilo kwa ufanisi, bila kuondoa dhima na nia njema ya kuanzishwa kwa kiwanda hicho na Rais wa kwanza wa Tanzania, Hayati Julius Nyerere, ambayo ilikuwa ni kuiwezesha Serikali kupata mapato pamoja na kuzalisha ajira kwa Watanzania.

Balozi Salum alitoa agizo hilo alipohitimisha ziara yake ya kutembelea Kiwanda cha General Tyre (Arusha) pamoja na Kiwanda cha Kilimanjaro Machine Tools (KMTC) kilichopo Mkoa wa Kilimanjaro, Aprili 27, 2026. Alisema Serikali, kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara, itafanya tathmini ya kina ili kubaini uwekezaji bora katika eneo hilo, ikiwemo uwekezaji wa viwanda au biashara kulingana na mapendekezo ya kamati hiyo.

Aidha, amesema ripoti ya kamati hiyo itasaidia kumshauri Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga, kuhusu aina bora ya uwekezaji katika eneo hilo lenye ukubwa wa ekari 54, kwa kuzingatia maono ya mwanzilishi wa kiwanda hicho, Hayati Julius Nyerere, pamoja na kuhifadhi historia yake.

Kwa upande wa Kiwanda cha Kilimanjaro Machine Tools, Balozi Salum amesema Wizara itahakikisha kuwa katika Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2026/2027 inatenga fedha za kutosha kwa ajili ya kuongeza mashine za kisasa. Hatua hiyo itawawezesha vijana wengi wa mikoa ya Kaskazini kujifunza na kupata ujuzi utakaowasaidia kujiajiri.

Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuwahamasisha wamiliki wa viwanda visivyofanya kazi kuvifufua, ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, ya kuhakikisha viwanda vyote vinafufuliwa ili kuongeza ajira kwa vijana.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!