
Mgombea ubunge wa Jimbo la Kisarawe kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Seleman Jafo, ameweka wazi kwamba dhamira yake ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2030 Kisarawe inakuwa wilaya ya mfano Tanzania, yenye huduma za kijamii zinazofikika kwa kila mwananchi.
Katika maelezo yake, amesema lengo kuu ni kuona vijiji vyote vya Kisarawe vinakuwa na zahanati, ili kila mwananchi apate huduma za afya akiwa kijijini kwake. Ameeleza kuwa ndani ya siku 100 baada ya uchaguzi, wananchi wa Kijiji cha Mianzi watakuwa wanapata huduma za afya kijijini kwao, hatua ambayo ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa kuhakikisha kila kijiji kina zahanati.
Amefafanua zaidi kuwa Kisarawe imepiga hatua kubwa katika sekta ya elimu, ambapo awali kulikuwa na shule moja pekee ya kidato cha sita, lakini sasa zipo shule sita. Pia, kata zimepata shule mbili za sekondari, jambo ambalo halijawahi kutokea awali, likilenga kupunguza adha ya wanafunzi kutembea umbali mrefu.








