Home Kitaifa PROF. SHEMDOE: MAMEYA, WENYEVITI WA HALMASHAURI SIMAMIENI UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAENDELEO

PROF. SHEMDOE: MAMEYA, WENYEVITI WA HALMASHAURI SIMAMIENI UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAENDELEO

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Prof. Riziki Shemdoe amewasihi waheshimiwa Mameya na Wenyeviti wa Halmashauri nchini kuhakikisha wanaisaidia Serikali katika kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Prof. Shemdoe ametoa rai hilo leo tarehe 27 Juni, 2022 kwenye mafunzo ya Waheshimiwa Mameya na Wenyeviti wa Halmashauri zote yanayofanyika Jijini Dodoma.

Amesema Mamlaka za Serikali za Mitaa ndio injini wa Serikali, hivyo Mameya na wenyeviti wa Halmashauri wanawajibu wa kuhakikisha wanasimamia kwa karibu miradi ya maendeleo katika Halmashauri wanazozisimamia ili miradi hiyo iweze kukamilika kwa wakati.

“Serikali imeelekeza fedha nyingi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, hivyo ni wajibu wa viongozi hao kuhakikisha wanaisimamia kwa karibu ili iweze kukamilika kwa wakati na wananchi wapate huduma” amesisitiza Prof. Shemdoe

Aidha , amewashikuru waheshimiwa Mameya na Wenyeviti wa Halmashauri nchini kwa kushirikiana na viongozi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa katika kusimamia na ukamilishaji wa ujenzi wa madarasa 15,000 ambayo yamesaidia kupunguza upungufu wa madarasa nchini.

Mafunzo ya waheshimiwa Mameya na Wenyeviti wa Halmashauri yanafanyika kwa siku mbili ambapo mada zitakazotolewa ni Uongozi na Utawala bora, Sheria za uendeshaji wa Serikali za Mitaa na ugharamiaji wa miradi kwa kutumia vyanzo mbadala.

Pia watajengewa uwezo katika wajibu na majukumu ya waheshimiwa Mameya na Wenyeviti wa Halmashauri, mahusiano baina ya viongozi wa kisiasa na watendaji katika mamlaka za Serikali za Mitaa Usimamizi wa Mapato na matumizi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa na usimamizi wa miradi ya maendeleo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!