Home Kitaifa PROF. KITILA MKUMBO AKUTANA NA BODABODA KIBANGU NA KUZUNGUMZA NAO

PROF. KITILA MKUMBO AKUTANA NA BODABODA KIBANGU NA KUZUNGUMZA NAO

Waziri wa Nchi OR-MU na Mbunge wa Jimbo la Ubungo Prof. Kitila Mkumbo amefanya ziara katika Kata ya Makuburi na kukutana na waendesha pikipiki maarufu kama Bodaboda katika eneo la Kibangu ambao wameeleza changamoto zao na kumshukuru Mbunge wao kwa kuwatetea.

Waendesha pikipiki hao wakiongozwa na Frank Kaaya wamesema baada ya Prof. Kitila Mkumbo kuwasemea bungeni kuhusu kuingia mjini, baadhi ya changamoto zilipungua na kuomba wapatiwe mikopo ili waweze kumiliki vyombo vyao vya moto badala ya kuendesha vyombo vya watu wengine.

Aidha wamemuomba Mbunge wao awasaidie katika jeshi la polisi pale wanapokamatwa na makosa ya barabarani wapewe muda wa kulipa kama ilivyo kwa vyombo vingine vya moto badala ya kutakiwa kulipa faini papo kwa hapo jambo ambalo linawawia vigumu.

Waendesha pikipiki hao pia wameomba kurahisishiwa utaratibu wa kujiunga na Bima ya Afya.

Akijibu hoja hizo Prof. Kitila Mkumbo amewataka waendesha pikipiki hao kujiunga katika vikundi na kuvisajili ili mikopo itakapoanza kutolewa na wao wapate na kulikabidhi jukumu hilo kwa Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa wa Kibangu.

Kuhusu Bima za Afya Prof. Kitila Mkumbo amesema tayari sheria ya afya kwa wote imeshatungwa ambayo itawezesha kila mtanzania kuwa na Bima ya afya na kinachoangaliwa kwa sasa ni watu wangapi hawana uwezo wa kujilipia ili walipiwe na Serikali.

Wakati zoezi hilo likiendelea Prof. Kitila Mkumbo amewashauri waendesha pikipiki hao kukata Bima ya CHF ambayo Diwani wa Kata ya Makuburi ameahidi kusimamia zoezi hilo ambalo kadi zake zinaruhusu kutibiwa mpaka katika Hospitali za mkoa.

Changamoto ya makosa ya barabarani na utaratibu wa utizaji wa faini, Mbunge huyo ameahidi kulifanyia kazi.

= = = = = =

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!