Na. Yusuph Mussa, Korogwe
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Korogwe Mjini mkoani Tanga Thobias Nungu amesema Benki ya NMB bado ni kimbilio la Watanzania wengi katika kupata huduma bora za kibenki.
Aliyasema hayo Oktoba 5, 2022 kwenye hafla fupi iliyoandaliwa na Benki ya NMB Tawi la Korogwe ikiwa ni Wiki ya Huduma kwa Wateja, na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa benki hiyo.
Nungu ambaye alikuwa ni mfanyakazi wa NMB Tawi la Korogwe miaka kadhaa iliyopita, alisema hata shughuli zake za ujasiriamali anazofanya, anaitumia benki hiyo kuhifadhi fedha, na shughuli nyingine.
“Mimi sikuja hapa kama mteja, bali pia ni mwana familia wa Benki ya NMB. Shughuli zangu zote ninazofanya nategemea Benki ya NMB. Hivyo nina hakika benki hii bado ni tegemeo kwa wananchi wengi” alisema Nungu ambaye amechaguliwa Oktoba 2, mwaka huu kuwa Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Korogwe Mjini”
Naye Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Korogwe Anisia Mauka, alisema ukiacha walimu na watumishi wa jumuiya hiyo, wanafunzi wake ni wateja wakubwa wa benki hiyo, na wamekuwa wakiridhika na huduma zinazotolewa na benki hiyo.
Meneja wa Huduma kwa Wateja wa Benki ya NMB Tawi la Korogwe Mwansiti Wakili, alisema benki hiyo imekuwa inafanya maboresho siku hadi siku. Nia ni kuwasogezea huduma kwa karibu zaidi wananchi na wateja wake.
“Sasa hivi Benki ya NMB ipo mkononi kwako. Huduma zote za kifedha zinafanyika kwenye simu yako. Hivyo mwananchi na mteja wetu unatakiwa kujivunia benki yako ya NMB ambayo imekurahisishia kupata huduma za kibenki kwa kidijitali zaidi” alisema Mwansiti.
Meneja wa NMB Tawi la Korogwe Lugano Mwampeta aliwashukuru Watanzania kwa kuwaunga mkono katika utoaji huduma, huku akitoa shukrani kwa wateja walioalikwa kwenye hafla hiyo, na kuahidi kutoa huduma iliyotukuka kwa Watanzania.