Home Kitaifa NEMC YATUNUKU TUZO SHULE BORA ZA UHIFADHI WA MAZINGIRA DSM

NEMC YATUNUKU TUZO SHULE BORA ZA UHIFADHI WA MAZINGIRA DSM

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limetoa tuzo na vyeti kwa shule za Msingi zinazofanya vizuri katika uhifadhi na usimamizi wa mazingira katika Mkoa wa Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yaliyofanyika Kimkoa Juni 5, 2026 katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam, yakiongozwa na kauli mbiu isemayo, “Dira 2050: Tuwajibike Kukijanisha Tanzania.”

Akizungumza katika Kilele cha Maadhimisho hayo, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Edward Mpogolo, ametoa wito kwa wananchi kuendelea kushiriki kikamilifu katika shughuli za uhifadhi na usimamizi wa mazingira ili kuhakikisha Tanzania inakuwa salama na endelevu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Amesema utunzaji wa mazingira ni msingi muhimu wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi, huku akisisitiza umuhimu wa kuwajengea vijana na wanafunzi utamaduni wa kulinda mazingira tangu wakiwa wadogo.

“Tunahitaji kuongeza juhudi za pamoja katika kulinda mazingira yetu, kwani mafanikio ya Dira 2050 yanategemea namna tunavyohifadhi rasilimali za mazingira na kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi,” amesema Mhe. Mpogolo.

Kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Kaimu Meneja wa Kanda ya Ilala, Bi. Zainab Kuhanwa, amesema kuwa NEMC kwa kushirikiana na KPMG Advisory Limited iliandaa mashindano maalum kwa shule za msingi za Mkoa wa Dar es Salaam kwa lengo la kutambua na kuthamini juhudi zinazofanywa na shule hizo katika kuhifadhi mazingira na kujenga kizazi chenye mwamko wa kulinda rasilimali za asili.

Ameeleza kuwa mchakato wa kupata washindi ulifanywa na timu ya wataalamu kutoka NEMC na KPMG kwa kuzingatia vigezo mbalimbali ikiwemo uwepo wa klabu hai za mazingira, walimu wa mazingira, upandaji na utunzaji wa miti, bustani za maua, usimamizi na utenganishaji wa taka, maeneo ya kuhifadhi taka, mabango ya elimu ya mazingira pamoja na usafi wa vyoo.

Bi. Kuhanwa amebainisha kuwa utoaji wa tuzo na vyeti hivyo kwa shule kumi bora ni sehemu ya jitihada za kuhamasisha wanafunzi, walimu na jamii kwa ujumla kuendeleza utamaduni wa kuhifadhi mazingira.

Amesema hatua hiyo inalenga kuwajengea wanafunzi uwezo wa kuwa mabalozi wa mazingira katika jamii zao na kuhamasisha wadau wengine kuiga mifano bora ya usimamizi wa mazingira kwa ajili ya maendeleo endelevu ya Taifa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!