Na Allawi Kaboyo – Bukoba.
Mkuu wa mkoa wa Kagera Albert Chalamila amedhamilia kuwatumia wasomi na wataalamu wa mkoa wa huo kuhakikisha anauendeleza kiuchumi na kidipLomasia.
Chalamila ametoa kauli hiyo Agosti 04, mwaka huu ikiwa ni mara ya kwanza tangu ateuliwe na kuapishwa kuwa mkuu wa mkoa wa Kagera, mara baada ya kukabidhiwa ofisi na mtangulizi wake Meja Jenerali Charles Mbuge katika hafla iliyofanyika ukumbi wa mkuu wa mkoa wa Kagera.
Amesema kuwa ili kuifikia adhima ya Rais Samia ya kuhakikisha mkoa huu unakua kiuchumi atahakikisha anawatumia wasomi ambao ni wazawa wa mkoa huu ambao wataweza kumpatia mawazo ya namna bora ya kufanikisha hilo.
“Mkoa huu unao wasomi wengi, wapo maprofesa, madaktari na watafiti wengi, nitawatumia wataalamu hao kupitia tafiti zao kuhakikisha mkoa huu tunauendeleza kiuchumi ili kufikia adhima ya Mhe. Rais Samia ya kuufungua mkoa huu kiuchumi.” Amesema Chalamila.
Kuhusu mipaka ya mkoa huu Chalamila amesema kuwa atahakikisha ulinzi unaimarishwa hususani kwa nchi zinazopakana na mkoa huu.
Amesema kuwa kutokana na mkla huu kupakana na nchi za jumuiya ya Afrika Mashariki hivyo atatumia fursa hiyo kuufungua mkoa huo kidiplomasia na kuhakikisha wananchi wan chi hizo wananufaika na mipaka yao.
Kwa upande wake aliyekuwa mkuu wa mkoa Kagera Meja Jenerali Charles Mbuge amemsihi mkuu mpya wa mkoa kuhakikisha anasimamia miradi ya maendeleo katika mkoa huo.
Jenerali Mbuge amemtaka mkuu mpya wa mkoa huo kuhakikisha anasimamia miradi yote ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa na kukamilika kwa wakati na kuendana na thamani ya fedha iliyotolewa huku akimkumbusha kusimamia zao muhimu la Kahawa.
Toba Nguvila Katibu tawala mpya wa mkoa wa Kagera amewataka wakuu wa wilaya na wakurugenzi kuendelea kumpa ushirikiano ili kuweza kufanikisha masuala mbalimbali ya mkoa huo.
Ameongeza kuwa yeye kama Katibu tawala alikuwa mkuu wa wilaya Muleba na sasa anaongoza mkoa mzima atahakikisha yale yote yaliyoshindikana yanawezekana kwa kushirikiana na watumishi wenzake.