Na Allawi Kaboyo Missenyi.
Naibu katibu mkuu wizara ya Maji Mhandisi Nadhifa Kemikimba ameagiza kukamilishwa na kuanza kutoa huduma ya maji miradi yote inayotekelezwa kwa fedha za Uviko-19 mkoani Kagera ifikapo tarehe 30 mwezi wa tisa mwaka huu.
Mhandisi Kemikimba amesema kuwa miradi hiyo ilitakiwa kuwa imekamilika mwezi juni kwa mujibu wa mikataba hivyo kutokamilika kwa wakati inapelekea wananchi kuendelea kupata adha ya maji tofauti na malengo ya serikali.
Kemikimba ametoa maagizo hayo alipotembelea mradi wa maji wa Buyango septemba 07 mwaka huu na kujionea hali ya utekelezaji wa mradi huo ambapo amemtaka mkandarasi kuongeza kasi ya utekelezaji ili malengo ya serikali ya kuwafikishia wananchi maji yanafikiwa.
“Nimejionea mwenyewe hali ya utekelezaji wa mradi huu ambao ulitakiwa kukamilika mwezi juni, ila kutokana na changamoto ambazo tayari tumeshazitatua naagiza miradi yote mkoani Kagera ukiwemo huu ikamilishwe kabla ya tarehe 30 mwezi huu.”
“Nimshukuru Mhe. Samia Suluhu Hassani Rais wa Tanzania ambaye kwa mapenzi yake ametupatia fedha hii, hivyo sisi kama wasaidizi wake kwenye sekta ya maji hatutakuwa kikwazo cha wanachi wa Buyango na Kagera kwa ujumla kupata maji safi na salama na yenye kutosheleza.” Amesisitiza Mhandisi Kemikimba.
Sambamba na hayo ameagiza kukabithiwa mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Buwasa vituo vya kuchotea maji vilivyokamilika vya mradi wa maji wa KYAKA-BUNAZI ili kuanza kutoa huduma ya maji kwa wananchi.
Kwa upande wake mkandarasi Athumani Mkono kutoka kampuni ya ADVANCED ENGENERING COMPANY LTD amesema kuwa sababu zilizopelekea kuchelewa kwa mradi huo ni kuchelewa kwa mambomba ambayo yananunuliwa na wizara, kuwepo kwa miamba kwenye njia za kupitisha mabomba hali iliyopelekea kutumia muda mrefu wa kuchimba mitaro sambamba na kuchelewa kwa fedha.
Awali kwenye taarifa ya utekelezaji wa mradi huo iliyotolewa na Meneja wa RUWASA wilaya ya Missenyi Mhandisi Andrew Kilembe imeeleza kuwa mradi huo unatekelezwa kwa gharama ya zaidi ya shilingi milioni 575.8 ambapo ameongeza kuwa hadi sasa mradi huo upo asilimia 85% ya utekelezaji wake.
Akiongea kwa niamba ya wananchi wa kata ya Buyango Mhe. Regina Lwamuganga diwani kata Buyango na Makamu mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya Missenyi, amesema kukamilika kwa mradi huo kutawasaidia wananchi wa kata hiyo hasa wakina mama ambao wamekuwa wakiteseka kufata maji mbali kwa zaidi ya kilomita 3.
Miradi ilittembelewa na naibu katibu mkuu wiara ya Maji Mhadisi Nadhifa Kemikimba ni mradi wa maji Buyango, Mradi wa maji Byamutemba na vituo vya kuchotea maji vya mradi wa maji KYAKA-BUNAZI.