Home Kitaifa MADIWANI MANISPAA YA BUKOBA WAILALAMIKIA TFS KWA KUWAKAMATA WAJASIRIAMALI.

MADIWANI MANISPAA YA BUKOBA WAILALAMIKIA TFS KWA KUWAKAMATA WAJASIRIAMALI.

Na Lilian Lugakingira
BUKOBA.

Madiwani wa halmashauri ya manispaa ya Bukoba mkoani Kagera wamemlalamikia Wakala wa Mistu Tanzania -TFS- kwa kuwakamata wajasiriamali wadogo wanaouza mkaa ndani ya manispaa hiyo, kwa madai kuwa wanaendesha biashara hiyo bila vibali.

Madiwani hao wametoa malalamiko hayo katika kikao cha nne cha kufunga mwaka wa fedha 2021/2022 na kusema kuwa wajasiriamali wanaokamatwa ni wale wanaouza mkaa kwa kupima makopo, ambao wanaununua kutoka kwa wauzaji wakubwa wenye vibali.

“Wasichezee jimbo letu na wasichezee kata zetu tumezitoa mbali, huo ndio msimamo wetu na wautambue hivyo, hali huko katika kata zetu ni mbaya kwa sababu ya watu hawa wa TFS” amesema diwani Ramadhan Kambunga wa kata Kashai.

Naye meya wa manispaa ya Bukoba, Godson Gibson amewataka TFS kushirikiana na madiwani kuitisha mikutano ya hadhara katika kata zote na kuelimisha wananchi juu ya sheria hiyo, badala ya kuingia mtaani na kukamata watu wakati hawana uelewa.

Baadhi ya wajasiriamali waliozungumzia suala hilo akiwamo Jonesia Damian wamesema kuwa gharama ya shilingi 50,000 wanayotakiwa kulipa ili kupewa kibali cha kuanzia gunia moja hadi matano, ni kubwa ikilinganishwa na faida wanayoipata katika biashara hiyo, na kuomba kupunguziwa au kusamehewa kabisa.

Akitoa ufafanuzi juu ya malalamiko hayo Mhifadhi Mistu kutoka TFS Wilaya ya Bukoba Mwanamina Bakari amesema kuwa kabla ya usajili kuanza tarehe 01 Julai mwaka huu, walipita na gari wakitangaza kuhusu sheria mpya na kuwataka wadau kwenda kujisajili.

“Kuna akina mama wengi walifika ofisini kujisajili wakakutana na mimi mwenyewe, wakaniomba hadi kusogeza siku kutoka ile ya tarehe 01 Julai wakidai hawana hela hiyo, nikawaambia andikeni barua waeleze mwezi gani watakuja kulipa, ikawa hivyo na mwitikio ukawa mkubwa, lakini pia tumepanga kukutana na wadau wote wa mazao ya mistu kwa mwaka huu wa fedha, tulisitisha zoezi hilo mpaka sensa ipite ndipo tuwaite” amesema Bakari.

Mwisho

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!