Home Kitaifa HALMASHAURI YA JIJI LA TANGA YAMWAGA MAMILIONI YA MIKOPO KWA MAKUNDI MAALUMU

HALMASHAURI YA JIJI LA TANGA YAMWAGA MAMILIONI YA MIKOPO KWA MAKUNDI MAALUMU

NA BONIFACE GIDEON, TANGA

Halmashauri ya Jiji la Tanga imekabidhi jumla ya shs.377 milioni ukiwa ni mkopo kwa vikundi 43 vya uzalishaji mali kwa kipindi cha mwaka 2022/23 huku kukitolewa angalizo la kurudisha kwa wakati ili vikundi vingine pia viweze kukopeshwa.


Katika sherehe ya makabidhiano ya mkopo huo zilizofanyika katika Shule ya Sekondari ya Ufundi, Tanga, mgeni rasmi Mstahiki Meya wa Jiji la Tanga, Abdarhaman Shiloo alivipongeza vikundi vyote vilivyokamilisha marejesho ya mikopo yao ya awali na hivyo kustahili kuongezewa, na pia kuvitaka vikundi vipya vilivyofanikiwa kupata katika awamu hii
kuitumia kwa makusudio yaliyoorodheshwa katika mikataba yao.

Natoa wito kwenu wote kuzitumia fedha hizo kwa uangalifu, uaminifu ili ziweze kuleta tija kwa wanavikundi wote na hatimaye muweze
kurudisha mikopo hiyo kwa wakati”
, alisema Shiloo.

Mstahiki Meya aliwakumbusha wanavikundi kwamba mikopo hiyo ni mtihani kwao kwani ni kipimo kitakachowapima uwezo wao wa kuongezwa au kupunguziwa mkopo. Alisema katika kipindi kilichopita cha mwaka 2021/22, serikali ya Halmashauri ya Jiji la Tanga ilitoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya shs.980 milioni kwa vikundi visivyopungua 20.

Vikundi hivyo vinajumuisha Vijana, Wanawake naWalemavu. Awali akimkaribisha Mstahiki Meya kukabidhi mikopo hiyo, Mkurugenzi wa
Jiji, Dr.Sipora Liana alifahamisha kwamba vijana 70 waliokopeshwa pikipiki za bodaboda kutoka kundi la Vijana wameingia “mitini” na kwamba hatua za kisheria zinatayarishwa ili wabanwe na kuzirejesha.

Kutokana na maelezo ya Dr. Liana, kitendo cha kuingia “mitini” vijana hao wa bodaboda, tayari wamejiondoa katika stahiki ya kukopesheka katika awamu hii.

Nao wafaidika wa mikopo hiyo, waliipongeza Serikali ya Awamu ya 6 kwa kuwajali wananchi kwa kutoa mikopo ili wajiendeleze, lakini wakawataka wafaidika wa mikopo hiyo kulipa kwa wakati uliokubalika ili watoe nafasi kwa wengine waweze kupata.

Rashidi Hussein wa kundi la Vijana kutoka Kindi Farmers Youth Group alisema wamepewa mkopo wa shs.milioni 40 ukilinganisha na kipindi kilichopita ambapo walipata mkopo wa shs.milioni 20 na kumudu kurudisha katika kipindi kifupi tu cha miezi mitatu. Kikundi
hujishughulisha na biashara ya kuuza mchele katika eneo maarufu lililopo barabara 16 jijini Tanga. Rashidi alisema wananunua mchele
kutoka mikoa ya Morogoro na Mbeya.

Wakati Seif Ally kutoka kundi la Walemavu akisema mkopo wao waliopatawatanunua bajaj watakazotumia kama bodaboda, Bora Charles Mkassa kutoka kundi la Wanawake, alisema watatumia mkopo wao kuendeleza biashara ya kufuga kuku wa mayai.


Vikundi hivyo vitatu vilivyopewa mikopo walipewa semina ya siku moja shuleni hapa zilizotolewa na taasisi za benki ili kuwanoa namna bora ya kufanya biashara zao kwa ufanisi. Benki hizo ambazo ndizo zilizowezesha mikopo hiyo ni Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), Benki ya NMB na benki ya CRDB.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!