Na Mercy Maimu
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, NAPE NNAUYE, amesema Serikali inaendelea kufanya mapitio ya gharama halisi ya huduma ya mawasiliano nchini ili kupunguza makali ya gharama za watumiaji wa internet nchini ambazo zimeendelea kulalamikiwa na Watu wengi.
Amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam na kuongeza kuwa zoezi hilo litakamilika Mwezi Desemba hivyo hakutakuwa na mabadiliko yoyote mpaka pale mchakato mzima utakapo kamilika.
“Serikali tumelishasema tangu awali kuwa tutashirikiana na wadau kuboresha kila eneo ambalo lina ukakasi, nia yetu ni kuweka mazingira bora kwenye sekta ya habari, tushirikiane kuijenga nchi yetu” amesema
Amesema Serikali imepokea mapendekezo ya marekebisho baada ya kufanyika kwa vikao mbalimbali kati ya watendaji na wadau na hatua inayofuata ni uandishi wa mapendekezo hayo.
“Zipo taratibu mbalimbali hadi muswada wa marekebisho uingie bungeni, hivi sasa tunazifuata, waandishi wa mapebdekezo wakikamilisha utapelekwa kwa watunga sheria” amesema.
Naye Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), DEODATUS BALIKEambaye ni miongoni mwa walioshiriki kwenye kikao hicho amesema kuna dalili nzuri za kuelekea kwenye marekebisho ya sheria hiyo.
Amesema vikao wanavyovifanya na watendaji wa Serikali pamoja na Waziri vinaonyesha dhamira njema waliyonayo na anamini kama mambo yatakwenda kama walivyokubaliana tasnia ya habari itakua.
‘‘Tunajua marekebisho hayawezi kufanya mara moja kuna hatua za kufuatwa, kikao kilikuwa kizuri, Serikali imeendelea kuonyesha dhamira yake” amesema Balile.
Balile amesema mabadiliko ya vifungu vya sheria lina mchakato wake ambao utaendelea baada ya wadau kupewa fursa na kutoa mapendekezo yao tofauti na ilivyokuwa huko nyuma.
Miongoni mwa mapendekezo ya CoRI kwa Serikali ni pamoja na mamlaka ya Mkurugenzi wa Habari (MAELEZO) yafutwe na kiundwe chombo ambacho kitashughulikia masuala ya usuluhishi yanapotolewa malalamiko dhidi ya chombo cha habari, badala ya kazi hiyo kufanywa na mtu mmoja.
Wadau wanataka marekebisho dhidi ya kifungu cha 6 (e) kinachoelekeza magazeti kupatiwa leseni badala ya usajili wa moja kwa moja.Pia wadau hao wanapendekeza magazeti yasiendeshwe kwa kupewa leseni kila mwaka, badala yake yapewe usajili wa kudumu au wa muda mrefu, ili kudhibiti utaratibu wa kufuta leseni kiholela.
Mapendekezo mengine kuhusu sheria hiyo, ni marekebisho dhidi ya kifungu chake cha 7 (2)(b)(lV), kinachoelekeza vyombo vya habari kutangaza au kuchapisha habari na masuala yenye umuhimu kwa taifa, kadiri itakavyelekezwa na serikali, wadai wakieleza kipengele hiki kinaingilia uhuru wa uhariri.
Sheria nyingine zinazolalamikiwa ni Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Huduma za Posta (EPOCA, 2010), Sheria ya Makosa Mtandaoni (2015), Sheria ya Haki ya Kupata Habari (2016) na Kanuni za Maudhui Mtandao (2018) kama zilivyorekebishwa mara kadhaa.