Home Kitaifa DKT MKILIA : ” USAJILI WA LAZIMA WAANZA , TUME YA ULINZI...

DKT MKILIA : ” USAJILI WA LAZIMA WAANZA , TUME YA ULINZI WA TAARIFA BINAFSI KUCHUKUA HATUA ZA KISHERIA KWA WATAKAOKIUKA ” .

 Na Mwandishi Wetu.

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC), Dkt. Emmanuel Mkilia, ametoa wito kwa taasisi zote zinazokusanya au kuchakata taarifa binafsi kuhakikisha zinazingatia matakwa ya Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, Sura ya 44, huku akisisitiza kuwa utekelezaji kamili wa sheria hiyo umeanza na hatua za kisheria dhidi ya wanaokiuka masharti yake zinaendelea kuchukuliwa.

Dkt. Mkilia amesema hatua hizo zimeanza tangu Aprili 9, 2026 baada ya kukamilika kwa kipindi cha usajili wa hiari tarehe Aprili 8, 2026.

Kwa mujibu wa sheria hiyo, ni marufuku kwa taasisi yoyote kukusanya au kuchakata taarifa binafsi bila kusajiliwa na Tume kama Mkusanyaji na/au Mchakataji wa Taarifa Binafsi. Taasisi zitakazobainika kufanya shughuli hizo bila usajili zitakuwa zinatenda kosa la kisheria na zinaweza kuchukuliwa hatua mbalimbali za kisheria na kiutawala, ikiwemo kutozwa faini kwa mujibu wa sheria.

Dkt. Mkilia amesema Tume inazitambua na kuzipongeza taasisi zote zilizokamilisha usajili wao katika kipindi cha hiari.

“Mpaka Aprili 8, 2026, zaidi ya taasisi 14,000 zilikuwa zimejisajili. Huu ni mwitikio mzuri unaoonesha dhamira ya wadau katika kulinda faragha na taarifa binafsi za wananchi,” amesema.

Aidha, ametoa maelekezo kwa taasisi ambazo bado hazijakamilisha au kuanza mchakato wa usajili kuhakikisha zinakamilisha taratibu hizo ndani ya siku saba za kazi kuanzia Juni 12, 2026.

“Taasisi zote zilizoanza mchakato wa usajili lakini hazijaukamilisha zinapaswa kuukamilisha ndani ya siku saba za kazi. Vilevile, taasisi ambazo bado hazijaanza kabisa mchakato wa usajili zinatakiwa kuanza na kuukamilisha ndani ya muda huo,” amesema.

Ameongeza kuwa taasisi zote zinapaswa kujiandaa kwa ukaguzi wa uzingatiaji wa sheria ambao tayari umeanza, pamoja na kuhakikisha zinakuwa na sera zilizoidhinishwa za ulinzi wa taarifa binafsi na mifumo madhubuti ya kulinda taarifa hizo.

Wakati huo huo, Dkt. Mkilia amewaalika wadau mbalimbali kujiandikisha na kushiriki Kongamano la Kwanza la Taifa la Faragha na Ulinzi wa Taarifa Binafsi litakalofanyika kuanzia Juni 29 hadi Julai 2, 2026 katika Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.

Amesema kongamano hilo litawakutanisha wataalamu, watunga sera, wasimamizi wa sheria, sekta binafsi, watafiti na wadau wengine kutoka ndani na nje ya nchi kujadili masuala ya faragha, ulinzi wa taarifa binafsi na mustakabali wa huduma za kidijitali.

“Maafisa Ulinzi wa Taarifa Binafsi na timu zao wanahimizwa kushiriki kongamano hili muhimu ili kujenga uelewa, kubadilishana uzoefu na kujifunza kutoka kwa wataalamu na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi,” amesema.

Ameeleza kuwa kongamano hilo litatoa fursa ya kujadili teknolojia zinazoibukia, changamoto za ulinzi wa taarifa binafsi katika mazingira ya kidijitali, pamoja na kuimarisha ushirikiano unaohitajika katika kujenga Tanzania yenye huduma za kidijitali salama, zinazoaminika na jumuishi, sambamba na maono ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!