Leo Agosti 29, 2022 Mahakama ya Wilaya ya Ludewa imemtia hatiani mtu mmoja anae julikana kwa majina ya John Sevelini Chale (60) Mkazi wa Kijiji cha Iwela Wilaya ya Ludewa kwa kosa la kukutwa na hatia ya Uchawi na kuhukumiwa kwa kifungo cha miaka mitano (5) Jela.
Mnamo tarehe 01/02/2022 majira ya saa 08:30 asubuhi katika kijiji cha Iwela Wilaya ya Ludewa mkoa wa Njombe ziliripotiwa taarifa kwamba mtuhumiwa anatuhumiwa kwa kujihusisha na vitendo vya kishirikina toka kwa mlalamikaji aitwaye Hekima Antony Chale ambaye ni kaka wa mhanga Vediana Antony Chale ambaye ni mtoto wa mdogoake mtuhumiwa vilivyo pelekea kuugua kichaa,
Kwa mujibu wa taarifa za shitaka hilo leo Mahakamani zinasema baada ya upelelezi kukamilika mtuhumiwa alifikishwa katika Mahakama ya Wilaya Ludewa tarehe 01/03/2022 ambapo alisomewa shitaka moja la kujihusisha na vitendo vya kishirikina kwa mujibu wa kinyume na kifungu 3(a) na 5(1) cha sheria ya uchawi sura ya 18 marejeo 2019 na mwendesha mashtaka wa serikali Asifiwe Asajile mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Ludewa Mhe. Isaac Ayeng’o.
Hivyo baada ya mahakama kusikiliza pande zote mbili ilijiridhisha kuwa upande wa mashtaka umeweza kuthibitisha kosa bila kuacha shaka yoyote hivyo ilimkuta mshitakiwa na hatia.
Mwendesha mashtaka wa serikali iliiyomba Mahakama kumpatia mshitakiwa adhabu kali ili iwe fundisho kwake na jamii kwa ujumla kwani vitendo vya kishirikina vinasababisha migogoro ya familia na jamii kwa ujumla na hata kupelekea mauaji na baada ya hoja hizo Mahakama ilimuhamuru mshitakiwa kutumikia kifungo cha Miaka 5 Jela.