Agizo la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi limetekelezwa kwa Vitendo Unguja na Pemba
Ameyasema hayo Waziri wa Nchi, Afisi ya Rais Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Mhe Mudrik Ramadhan Soraga wakati akijibu swali la Mwakilishi wa Jimbo la Mtambwe Mhe. Habib Ali Mohammed juu ya hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa agizo la Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi la kuwawezesha Wananchi Kiuchumi kupitia mikopo ya fedha za Ahueni ya Uviko 19 inayotolewa chini ya Wizara yake, katika kikao cha nne (4) cha Baraza la kumi la Wawakilishi huko Chukwani Mkoa wa Mjini Magharib Unguja
Amesema hadi kufikia mwezi agosti mwaka huu jumla ya mikopo 1427 kwa vikundi na mtu mmoja mmoja imetolewa kwa Unguja na Pemba yenye thamani ya shilingi za Kitanzania Bilioni 10.3 ambapo zaidi ya wananchi elfu 23 wamenufaika na mikopo hiyo kwa wanawake na wanaume
Ameongeza kuwa kupitia mikopo hiyo Wananchi wengi wamejipatia ajira katika sekta mbali mbali ikiwemo Ufugaji, biashara za maduka ya jumla na reja reja, Kilimo pamoja na Ufundi Seremala.