


Na. Josephine Majura, WF, Dar es Salaam.
Jumla ya wakaguzi 120 wa ndani wa taarifa za fedha wamepatiwa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kukagua taarifa za fedha ili kuhakikisha taarifa za fedha zinaandaliwa kwa viwango vya kimataifa.
Akizungumza wakati wa Kufunga mafunzo hayo, Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali, Bw. Benjamin Magai, alisema kuwa mafunzo hayo yamelenga kuboresha utendaji wa wakaguzi wa ndani ili kuzishauri menejimenti za taasisi husika kuhusu usahihi wa taarifa hizo kabla hazijawasilishwa kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Bw. Magai, aliongeza kuwa Taarifa za fedha zinapaswa kuandaliwa kwa kuzingatia viwango vya kimataifa vya uandaaji wa hesabu na miongozo ya Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi ikiwa ni pamoja na kupunguza hoja za ukaguzi ambazo zimekuwa zikitolewa mara kwa mara na CAG.
“Ni matarajio yangu kuwa kupitia mafunzo haya mtakuwa mmeelewa namna bora ya kukagua Taarifa za Fedha za taasisi zenu hali itakayopelekea kutoa ushauri stahiki utakaowezesha kuboreshwa kwa taarifa husika kabla ya kukamilika kwa ukaguzi wa CAG”, alisema Bw. Magai.
Aidha, Bw. Magai aliwataka wakaguzi waliohudhuria mafunzo hayo kupeleka pia ujuzi kwa wale ambao hawakuweza kushiriki waweze kupata maarifa na kufanya vizuri katika taasisi zao na Wizara kupitia ofisi ya Mkaguzi wa ndani mkuu wa serikali itafanya ufuatiliaji wa ufanisi wa ukaguzi wa taarifa hizo kwa taasisi zote ambazo zimepatiwa mafunzo ili kutathmini utekelezaji wa jukumu hilo.
Mafunzo hayo yaliendeshwa kwa awamu mbili ambapo kila awamu ikiwa na wakaguzi wa ndani 60.
MWISHO








