Home Kitaifa WAZIRI MKENDA AUNDA TUME KUCHUNGUZA UTOAJI MIKOPO KWA WANAFUNZI ELIMU YA JUU

WAZIRI MKENDA AUNDA TUME KUCHUNGUZA UTOAJI MIKOPO KWA WANAFUNZI ELIMU YA JUU

Na Mathias Canal, WEST

Wakati dirisha la maombi ya mikopo kwa mwaka wa masomo 2022/2023 likiwa wazi kwa muda wa siku 70 kuanzia Julai 19 hadi Septemba 30 mwaka huu, Serikali imetangaza Tume ya watu watatu kuchunguza utoaji wa mikopo.

Tume hiyo itaongozwa na Prof Allan Mushi ambaye ni mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe Morogoro, Idd Makame kutoka Zanzibar na Dkt Martin Chegeni ambao wote kwa pamoja ni wataalamu wa mifumo waliobobea katika sayansi ya Kompyuta na Takwimu.

Tume hiyo itachunguza uhalali katika utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2017/2018 mpaka 2021/2022 ili kubaini kama kulikuwa na upendeleo kwa watu wasiokuwa na sifa.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda ametangaza tume hiyo tarehe 29 Julai 2022 Jijini Dar es laam wakati akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari nchini juu ya mwelekeo wa Wizara, Vipaumbele na maeneo ya kimkakati katika utekelezaji kwa Mwaka wa fedha 2022/23.

Waziri Mkenda amesema kuwa Tume hiyo itapitia malalamiko ya wanafunzi mbalimbali nchini ambao wamekuwa wakiyatoa kuhusu upendeleo wa utoaji mikopo kwa kupata mikopo kwa wanafunzi wenye sifa huku wale wasiokuwa na sifa stahiki wakikosa mikopo hiyo.

“Na kwenye hili tunakaribisha watu watoe taarifa kwa sababu kama kuna mtoto wa Mkenda uliyesoma nae utakuwa unamjua baba yake ni nani na uwezo wake, halafu wewe unaona mtu huyo amepewa mkopo toa taarifa” Amekaririwa Waziri Mkenda na kuongeza kuwa

“Mtu yeyote ambaye ana wasiwasi na utoaji wa mikopo tunamkaribisha ili aweze kuisaidia tume kufanya kazi yake kwa kuwa na taarifa zenye usahihi wa hali ya juu kutoka kwa wanachi husika”

Prof Mkenda amesema kuwa tume hiyo itaangalia vigezo vilivyoainishwa ili kuona kama kuna taarifa zingine za ziada zinaweza kutumika katika utoaji wa mikopo ili fedha zinazotolewa na serikali zikopeshwe kwa haki.

Kadhalika, Waziri Mkenda amewahimiza waombaji mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka 2022/2023 kusoma na kuuzingatia ‘Mwongozo wa Utoaji Mikopo kwa mwaka 2022/2023’ ili kuwasilisha maombi kwa usahihi ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa sahihi zilizowekwa kwa mujibu wa taratibu na sheria.

Katika mwaka wa masomo 2022/2023, Serikali imetenga kiasi cha TZS 573 bilioni kwa ajili ya kutoa mikopo na Udhamini (Scholaship) kwa wanafunzi wa elimu ya juu nchini.

Mwisho

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!