
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema Mashindano ya Bunge Marathon yamekuwa ni jukwaa la Kimataifa linalounganisha na kuwaweka pamoja watu mbali mbali kupitia michezo.
Ameyasema hayo katika mashindano ya Bunge Marathon 2026 yaliyofanyika katika Uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.
Amesema lengo la kufanyika kwa mashindano ya Bunge Marathon ni kuendeleza ushirikiano na mshikamano uliopo kati ya watumishi wa Serikali wakiwemo wabunge na wananchi katika kuhakikisha wanaishi kwa kuvumiliana, kushirikiana na kujenga nidhamu ya kujituma wakati wowote wawapo katika majukumu ya kiserikali na kijamii.
Aidha, Mhe. Hemed amefahamisha kuwa Marathon ni nyenzo inayounganisha Taasisi na jamii katika kujenga afya bora na urafiki ambao utaliwezesha Taifa la Tanzania kuwa na watu wenye afya bora, upendo na mshikamano wa kudumu.
Sambamba na hayo Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar ametoa raia kwa wananchi kuandaa utaratibu wa kufanya mazoezi kwa kutambua kuwa wananchi wenye afya bora ni mtaji katika kuongeza nguvu ya uzalishaji na kuliletea Taifa maendeleo.
Hata hivyo amewakumbusha wananchi wote kuendelea kuilinda amani ya nchi kwa kuishi kwa umoja, upendo, mshikamano na kuheshimiana ili Tanzania izidi kupiga hatua zaidi kimaendeleo.
Nae Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. MUSSA AZZAN ZUNGU (Mb) amemshukuru Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa kuendelea kushirikiana nao katika Mashindano hayo jambo linalodhihirisha upendo na mshikamano alionao kwa Watanzania na utayari wake wa kulitumikia Taifa muda wowote.
Mhe. Zungu amewapongeza wadhamini wa mashindano hayo kwa kuridhia kudhamini mashindano hayo ambayo yamefanikiwa kwa viwango vya hali ya juu na kuwataka kuendelea kushirikiana na Bunge ili kuhakikisha mashindano hayo yanaendelea kufanyika kwa ufanisi mkubwa zaidi.
Kwa upande wake Mwnyekiti wa kamati ya maandaliza ya Bunge Marathon Mhe. FESTO SANGA amesema lengo la kamati ni kuhakikisha wanatanua wigo mkubwa zaidi na kuyapa hadhi mashindano hayo ambayo yamekuwa ni kiunganishi kati ya Watumishi wa Serikali na wananchi kutoka Mikoa mbalimbali na kutoa fursa zaidi za kiuchumi na kijamii.
Amesema Kamati hio itaendelea kufanya kazi kwa mashirikiano, uzalendo na ubunifu mkubwa ili mashindano ya Bunge Marathon yaendelee kulinda hadhi ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuitangaza Tanzania Kitaifa na Kiimataifa.
Mapema Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya SILENT OCEAN LIMITED ambao ndio wadhamini wakuu wa mbio za Bunge Marathon ndugu MOHAMMED SOLOKA amesema kampuni hio itaendelea kudhamini mashindano hayo na kuhakikisha yanafanyika kwa ufanisi na viwango vya hali ya juu.
Ndugu Mohammed amewataka Watanzania kuendelea kufanya mazoezi ili kujenga Afya ya mwili na akili lakini pia kuhakikisha Taifa linakuwa na watu wenye Afya watakaosaidia katika harakati mbalimbali za kuliletea Taifa Maendeleo.
Imetolewa na Kitengo cha Habari ( OMPR )
Leo tarehe 18 / 04 / 2026








