WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema ukarabati mkubwa uliofanyika kwenye uwanja wa Mpira wa Miguu wa Majaliwa uliopo Ruangwa mkoani Lindi umekamilika kwa asilimia 98 na utakuwa tayari kutumika kwa mechi za Ligi kuu Tanzania Bara.
Majaliwa amewashukuru wananchi wa Ruangwa kwa kukubali kuchangia shilingi 20/-, kwa kila kilo ya mazao waliyouza ambayo imewezesha Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa kukusanya kiasi cha milioni 200 zilizowezesha kununua nyasi bandia.
Amesema hayo jana (Ijumaa, Agosti 19, 2022) wakati akikagua maendeleo ya ukarabati wa uwanja huo ambao umejengwa kwa viwango vya kimataifa, wilayani Ruangwa mkoani Lindi.
“Hakuna maendeleo yanayoweza kupatikana mahali bila wewe mwenyewe kuwa msitari wa mbele, wana Ruangwa nyie mmefanya maamuzi mazuri, siyo tu kwenye uwanja bali kwenye maeneo mengi na kwa kweli mmepata mafanikio. Hongereni sana.”
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amewapongeza viongozi wa Halmashauri hiyo kwa kusimamia ukarabati huo ambao utaleta tija kwa timu ya Namungo pamoja na timu nyingine za Mkoa wa Lindi.
Awali akitoa taarifa ya ukarabati huo, Mhandisi wa viwanja kutoka kampuni ya Azam, Bw. Victor Ndozelo amesema uwanja huo utakapokamilika kwa asilimia 100 utakuwa moja kati ya viwanja bora nchini na tayari wameandaa utaratibu wa kuomba kibali kutoka kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini na lile la soka Barani Afrika (CAF) ili pia uwanja huo uweze kutumika kwa michezo ya kimataifa.