
Wananchi wa wilaya ya Korogwe, mkoani Tanga, wameanza kuona mwanga mpya wa maisha kufuatia kuendelea kwa mpango wa usambazaji na uuzaji wa mitungi ya gesi ya kilo sita kwa bei ya ruzuku unaotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Mpango huo unaolenga kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia umeleta matumaini mapya kwa kaya nyingi zilizokuwa zikitegemea kuni na mkaa.

Katika muendelezo wa zoezi hilo, REA imeendelea kusambaza mitungi ya gesi kwa gharama nafuu, hatua inayolenga kuhakikisha hata wananchi wa kipato cha chini wanapata fursa ya kutumia nishati salama na rafiki kwa mazingira.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, msimamizi wa mradi kutoka REA, Ndugu Abdulrazack Mkomi, ameeleza kuwa jitihada hizo ni sehemu ya mkakati mpana wa serikali wa kupunguza utegemezi wa nishati za jadi ambazo zimekuwa zikichangia uharibifu wa mazingira na athari za kiafya.
“Serikali inayoongozwa na Dkt. Samia itaendelea kuhakikisha kila mwananchi anapata nishati safi ya kupikia. Hii si tu kuhusu urahisi wa maisha, bali pia ni kuhusu kulinda afya na mazingira yetu,” alisema Mkomi.
Baadhi ya wananchi walioanza kutumia gesi wameeleza kuridhishwa na mabadiliko hayo, wakibainisha kuwa matumizi ya gesi yamepunguza muda wa kupika, gharama za nishati na changamoto ya moshi majumbani.
“Zamani tulikuwa tunahangaika na kuni na mkaa, lakini sasa maisha yamekuwa rahisi zaidi. Gesi ni salama na haraka,” alisema mama mmoja mkazi wa Korogwe.
Mbali na usambazaji wa mitungi, REA pia imeendelea kutoa elimu ya matumizi salama ya gesi kwa wananchi, ikiwemo namna ya kuhifadhi mitungi, matumizi sahihi ya majiko na tahadhari za kuchukua ili kuepuka ajali. Hatua hiyo inalenga kuhakikisha kuwa matumizi ya nishati hiyo yanafanyika kwa usalama na ufanisi.
Kuendelea kwa mpango huu Korogwe kunatajwa kuwa hatua muhimu katika safari ya Tanzania kuelekea matumizi ya nishati safi, huku ukiwa chachu ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Kwa wakazi wa Korogwe, huu ni mwanzo wa zama mpya—zama za nishati safi, afya bora na mazingira yanayolindwa kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Mwisho








