Na.Alex Sonna-DODOMA
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amezindua rasmi ofisi za kampuni ya Landmax Real Estate Company Limited na kuzitaka Halmashauri pamoja na taasisi za umma kuongeza kasi ya utoaji huduma ili kuendana na mahitaji ya wawekezaji na kuchochea ukuaji wa uchumi.
Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi huo iliyofanyika Juni 24, 2026 jijini Dodoma, Senyamule amesema mafanikio ya sekta binafsi yanategemea kwa kiasi kikubwa mazingira rafiki yanayowekwa na Serikali kupitia huduma bora na za haraka.
Amesema Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 imeipa sekta binafsi nafasi kubwa katika kukuza uchumi wa nchi, hivyo ni muhimu kwa taasisi za umma kuhakikisha wawekezaji hawakwamishwi na urasimu au ucheleweshaji wa huduma.
“Tunapaswa kufanya kazi kwa kasi inayolingana na kasi ya wawekezaji. Kila huduma inayocheleweshwa ina athari kwa uwekezaji, ajira na maendeleo ya wananchi,” amesema Senyamule.
Amebainisha kuwa Mkoa wa Dodoma unaendelea kuvutia wawekezaji kutokana na nafasi yake kama makao makuu ya nchi, jambo ambalo limeongeza mahitaji ya ardhi, makazi na huduma mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
Kwa mujibu wake, ongezeko la uwekezaji katika mkoa huo limeifanya ardhi kuwa moja ya rasilimali muhimu zinazochangia ukuaji wa uchumi wa wananchi na Serikali kwa ujumla.
“Leo thamani ya ardhi Dodoma imeongezeka kwa kiwango kikubwa kutokana na kasi ya maendeleo. Ndiyo maana tunasema ardhi ni dhahabu ya Dodoma,” amesema.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Landmax Real Estate Company Limited, Onesmo Mnkondya, amesema kampuni hiyo imeanzishwa kwa lengo la kutoa huduma za kitaalamu katika sekta ya ardhi na mali isiyohamishika, sambamba na kusaidia kupunguza migogoro ya ardhi.
Amesema Landmax itatoa huduma za ununuzi na uuzaji wa ardhi, ushauri wa uwekezaji, usimamizi wa mali, urasimishaji wa nyaraka za ardhi, tathmini za soko na maendeleo ya miradi mbalimbali ya uwekezaji.
Kwa upande wake, Balozi wa Landmax ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Mjini, Clayton Chipando maarufu Baba Levo, amesema kampuni hiyo imejipanga kuhakikisha wananchi wanapata huduma salama na za uhakika katika miamala ya ardhi na nyumba.
Ameeleza kuwa matumizi ya huduma za kitaalamu yatasaidia kupunguza vitendo vya utapeli wa ardhi na kuongeza imani kwa wananchi wanaotaka kuwekeza katika sekta ya mali isiyohamishika.
Uzinduzi wa ofisi hizo unatajwa kuwa hatua muhimu katika kuimarisha huduma za ardhi na uwekezaji jijini Dodoma, ambalo linaendelea kukua kwa kasi na kuwa kitovu cha biashara na uwekezaji nchini.

























