Home Kitaifa RAIS SAMIA APOKEA GAWIO LA SH. BILIONI 15 KUTOKA TIPER

RAIS SAMIA APOKEA GAWIO LA SH. BILIONI 15 KUTOKA TIPER

Rais wa Jamhuri ya Muungwana wa Tanzania Dk.Samia Suluhu Hassan (katikati)akikabidhiwa gawio la Sh.bilioni 15 kutoka kwa  Mwenyekiti wa Bodi ya Tiper Balozi Mathias Chikawe(kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa Tiper  Mohamed Mohamed (kulia) wakati wa hafla ya Siku ya Gawio iliyofanyika Ikulu Dar es Salaam ambapo mashirika na taasisi mbalimbali ambazo Serikali inahisa wamekabidhi gawio serikalini.

****************

Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam

Kampuni ya Kuhifadhi Mafuta Tanzania (TIPER) imeikabidhi Serikali gawio la Shilingi bilioni 15 ikiwa ni sehemu ya gawio la rekodi la Shilingi bilioni 30 kwa wanahisa wake wawili, mafanikio yaliyotajwa kuchochewa na uwekezaji mkubwa katika miundombinu na ufanisi wa uendeshaji wa kampuni hiyo.

Makabidhiano hayo yamefanyika Ikulu jijini Dar es Salaam mbele ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa hafla ya mashirika na taasisi ambazo Serikali ina hisa kuwasilisha gawio kwa Serikali. TIPER, ambayo inamilikiwa kwa ubia wa asilimia 50 na Serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina na asilimia 50 na Oryx Energies, ilikabidhi jumla ya Shilingi bilioni 30 ambapo kila mwanahisa alipokea Shilingi bilioni 15.

Akizungumza katika hafla hiyo, Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu, alisema TIPER imefikia mafanikio makubwa mwaka huu kwa kutoa gawio kubwa zaidi katika historia ya kampuni hiyo.

“TIPER mwaka huu wameweza kuchangia gawio la Shilingi bilioni 15, ilhali mwaka 2025 hawakukidhi viwango. Hili ndilo gawio kubwa zaidi kuwahi kutolewa na TIPER,” alisema Mchechu.

Mkurugenzi Mtendaji wa TIPER, Mohamed Mohamed, alisema ongezeko hilo la gawio limetokana na uwekezaji wa zaidi ya Shilingi bilioni 105 uliofanywa katika kipindi cha miaka 10 iliyopita kuboresha matangi ya kuhifadhi mafuta, mifumo ya usambazaji, mifumo ya kuzima moto, umeme pamoja na kuongeza uwezo wa kuhifadhi mafuta kutoka lita milioni 253 hadi milioni 313.

Alisema mafanikio hayo pia yamechangiwa na mazingira mazuri ya uwekezaji yaliyowekwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambayo yameiwezesha kampuni kuongeza ufanisi na faida.

Mohamed alisema kati ya mwaka 2016 na 2020 Serikali ilipokea gawio la jumla la Shilingi bilioni 7.65 kutoka TIPER, lakini katika kipindi cha miaka mitano iliyofuata, kuanzia 2021 hadi 2025, gawio hilo limeongezeka hadi Shilingi bilioni 30.65, huku gawio la Serikali pekee likiongezeka kutoka Shilingi milioni 500 mwaka 2021 hadi Shilingi bilioni 15 mwaka 2025.

Alieleza kuwa fedha hizo zinazoingia Hazina Kuu zitasaidia kugharamia utekelezaji wa bajeti ya Serikali, ikiwemo ujenzi wa barabara, shule, hospitali, miradi ya umeme vijijini na huduma nyingine muhimu za kijamii.

Aidha, alisema kuanza kutumika kwa mfumo wa Single Receiving Terminal (SRT) wa mafuta ya dizeli Januari mwaka huu kumeongeza ufanisi katika upakuaji wa mafuta bandarini kwa kupunguza muda wa meli kutoka wastani wa siku tisa hadi siku nne, hatua iliyopunguza gharama za ucheleweshaji na kuongeza idadi ya meli zinazohudumiwa.

Mohamed alisema kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya huduma za kuhifadhi na kusafirisha mafuta ndani na nje ya Tanzania, kampuni imeandaa mpango wa kuwekeza zaidi ya Shilingi bilioni 265 katika miaka mitano ijayo ili kuongeza uwezo wa kuhifadhi, kupokea na kusafirisha mafuta na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara ya mafuta katika Afrika Mashariki na Kati.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!