
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amependekeza kuanzishwa kwa ushirikiano wa kindugu kati ya Zanzibar na Kisiwa cha Jeju, Jamhuri ya Korea (Korea Kusini), utakaolenga kuimarisha ushirikiano katika utalii endelevu, uchumi wa buluu, nishati mbadala, biashara na uwekezaji, pamoja na elimu na mafunzo.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 29 Oktoba 2026, alipokutana na Gavana wa Jeju, Mhe. Wi Seong-gon, kisiwani humo, akieleza kuwa Zanzibar inaweza kunufaika na uzoefu wa Jeju katika usimamizi wa utalii, matumizi ya nishati ya jua na upepo, uhifadhi wa mazingira na maendeleo ya uchumi wa bahari.

Aidha, amewakaribisha wawekezaji na wafanyabiashara wa Jeju kuangalia fursa za uwekezaji zilizopo Zanzibar, huku Gavana Wi Seong-gon akieleza utayari wa kuendeleza ushirikiano huo kupitia majadiliano ya kitaalamu na kuweka utaratibu wa kufuatilia hatua zinazofuata.










