
Na. Josephine Majura na Saidina Msangi, WF, Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Bw. Nsubili Joshua, amesema kuwa Mji wa Serikali Mtumba, ni moja ya jitihada za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania za kuboresha mazingira ya utendaji kazi wa taasisi za umma, kuimarisha uratibu wa shughuli za Serikali na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Bw. Joshua alisema hayo katika kikao na Wahariri wa Vyombo vya Habari, waliotembelea jengo la Wizara ya Fedha, kuelekea hafla ya Uzinduzi wa Majengo ya Ofisi, Wizara, Taasisi za Serikali na Barabara za Lami katika Mji wa Serikali Mtumba, mkoani Dodoma, itakayofanyika tarehe 30 Oktoba, 2026.

Alisema Mji huo una fursa ya kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi kwa kuongeza ufanisi na tija katika utendaji kazi kwa kuwa mazingira ya kisasa ya ofisi na miundombinu ya pamoja yanawezesha watumishi kutekeleza majukumu yao kwa tija, hivyo kuboresha ubora na kasi ya utoaji wa huduma.
‘‘Mji huu utapunguza urasimu katika utoaji wa huduma kwani ukaribu wa ofisi za Serikali unarahisisha mawasiliano, mashauriano na uratibu wa shughuli zinazohitaji ushirikiano wa kisekta, hivyo kusaidia kufanya maamuzi kwa wakati na kupunguza muda unaotumika katika kushughulikia maombi na mahitaji ya wananchi’’, alisema Bw. Joshua.

Bw. Joshua alisema mkusanyiko wa ofisi za Wizara katika eneo moja unarahisisha wananchi, wawekezaji na wadau wengine kufika na kupata huduma au kufanya mashauriano na taasisi mbalimbali za Serikali huku ukiimarisha uwazi na uwajibikaji katika kutoa huduma kwa wananchi.
‘‘Kuwepo kwa taasisi za Serikali katika eneo moja kutapunguza gharama za uratibu wa shughuli mbalimbali za Serikali pamoja na miundombinu ya kisasa kutoa fursa ya kuunganisha mifumo ya kidijitali ya Serikali, kurahisisha ubadilishanaji wa taarifa na kuwezesha wananchi kupata huduma kwa njia za kielektroniki’’, alifafanua Bw. Joshua.
Akizungumza kuhusu majukumu ya Wizara ya Fedha, Bw. Joshua alisema kuwa Wizara inasimamia Taasisi 35 zinazoratibu na kusimamia masuala ya fedha, uwekezaji wa mitaji ya Serikali, uwezeshaji wananchi kiuchumi ikiwemo soko la mitaji, dhamana na bidhaa, mafunzo ya elimu ya juu na kati, bodi za kitaalamu na kitaaluma, usimamizi wa kodi, ununuzi wa umma na michezo ya kubahatisha.
Alisema majukumu ya Wizara ni pamoja na kubuni na kusimamia utekelezaji wa sera za uchumi jumla, fedha na bajeti, ununuzi wa umma na ubia kati ya sekta ya umma na binafsi, kuandaa na kusimamia miongozo ya usimamizi wa bajeti ya Serikali pamoja na kuratibu upatikanaji wa misaada na mikopo nafuu na kuimarisha uhusiano na taasisi za kifedha za kikanda na kimataifa.
‘‘Wizara pia ina jukumu la kusimamia masuala ya mafao na pensheni kwa wastaafu wanaolipwa na Hazina, kusimamia masuala ya fedha na mali za Serikali, Kusimamia deni la serikali pamoja na Kusimamia masuala ya pamoja ya fedha kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar’’, alisema Bw. Joshua.
Aliongeza kuwa Wizara ya Fedha pia ina jukumu la kusimamia maendeleo ya sekta ya fedha, kusimamia takwimu rasmi za kitaifa pamoja na kudhibiti utakasishaji wa fedha haramu na ufadhili wa ugaidi.
Bw. Joshua alibainisha kuwa majukumu ya Wizara ya Fedha yanatekelezwa kupitia mafungu nane (8) ambapo mafungu sita (6) yapo ndani ya Wizara na Mafungu Mawili (2) ni taasisi zilizo chini ya Wizara.
Kwa upande wao Mhariri wa Gazeti la Habari Leo, Bw. Mgaya Kingoba, akizungumza baada ya kutembelea jengo la Wizara ya Fedha alisema kuwa jengo hilo ni moja kati ya majengo mazuri ambayo Serikali imejenga katika Mji wa Serikali Mtumba ikizingatiwa kazi zinazofanywa na Wizara hiyo.
‘‘Wizara ya Fedha ni kioo cha Serikali kwa sababu inakutana na mashirika ya kimataifa makubwa duniani ikiwemo Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo ya Afrika, Shirika la Fedha la Kimataifa na mengineyo, tumefurahishwa na jengo hili ambalo lina hadhi kubwa ikiwemo kumbi za mikutano zenye hadhi ya kuendesha vikao vya Baraza la Mawaziri.
Bw. Kingoba alipongeza juhudi za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa iliyofanyika katika Mji wa Serikali.
Bw. Kingoba alitoa rai kwa watumishi kutumia majengo hayo kuendelea kuboresha utendaji kazi na kuboresha utoaji wa huduma za Serikali kwa wananchi wote na kusisitiza wananchi watakaofika kupata huduma katika mji huo kuzingatia utunzaji wa miundombinu ili iweze kudumu kwa muda mrefu.
Ziara hiyo ya Wahariri wa Vyombo vya Habari kutembelea Jengo la Wizara ya Fedha lililo katika Mji wa Serikali Mtumba, iliratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu.
MWISHO.










