Home Kitaifa NEEC YAHITIMISHA MAFUNZO YA FURSA ZA MITAJI MKOA WA RUKWA

NEEC YAHITIMISHA MAFUNZO YA FURSA ZA MITAJI MKOA WA RUKWA

Baraza la Taifa la Uwezeshaji Kiuchumi (NEEC), kwa kushirikiana na Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Rukwa, Mhe. Jacquline Mzindakaya, limehitimisha mafunzo ya utoaji elimu kuhusu fursa za mitaji kupitia mifuko na programu mbalimbali za uwezeshaji wananchi kiuchumi yaliyofanyika katika halmashauri zote nne za Mkoa wa Rukwa.

Mafunzo hayo yalianza katika Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga, yakafuatiwa na Halmashauri za Wilaya za Nkasi na Kalambo, kabla ya kuhitimishwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Laela. Lengo la mafunzo hayo lilikuwa kuwawezesha wananchi kupata uelewa wa kina kuhusu fursa za mitaji, huduma za maendeleo ya biashara na programu mbalimbali za uwezeshaji zinazotolewa na Serikali na taasisi zake ili kujenga uchumi imara na unaojitegemea.

Akifunga rasmi mafunzo hayo kwa niaba ya Serikali, Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Laela, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Ndg. Missana Kalela Kwangura alisema kuwa elimu iliyotolewa na NEEC imekuja kwa wakati muafaka, kwani itaongeza uwezo wa wananchi kutambua na kutumia ipasavyo fursa zilizopo za kiuchumi kwa ajili ya kuongeza uzalishaji, ajira na kipato.

Alibainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji na ujasiriamali kupitia mifuko na programu mbalimbali za uwezeshaji, hivyo aliwataka washiriki kutumia elimu waliyoipata kuanzisha na kuendeleza miradi yenye tija kwa kuzingatia taratibu na usimamizi mzuri wa rasilimali.

Mkurugenzi Mtendaji huyo wa Wilaya aliipongeza NEEC kwa kuendelea kufikisha elimu ya uwezeshaji wananchi kiuchumi katika ngazi za jamii, akieleza kuwa hatua hiyo inaunga mkono juhudi za Serikali za kukuza uchumi shirikishi unaowanufaisha wananchi wa makundi yote.

Kwa upande wake, Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Rukwa, Mhe. Jackline Mzindakaya, alisema kuwa mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo wananchi, hususan wanawake, vijana na makundi maalumu, ili waweze kuzitambua na kuzifikia fursa zinazotolewa kupitia mifuko na programu mbalimbali za uwezeshaji.

Alisema ushirikiano kati ya NEEC, viongozi wa Serikali na wadau wa maendeleo umewezesha elimu hiyo kuwafikia wananchi katika halmashauri zote za Mkoa wa Rukwa, hatua ambayo itaongeza ushiriki wao katika shughuli za kiuchumi na kuchangia maendeleo ya mkoa na taifa kwa ujumla.

Naye mwakilishi wa Kaimu Katibu Mtendaji wa NEEC, Mkurugenzi wa Uwezeshaji na Ushiriki wa Watanzania Bi. Neema Mwakatobe alisema Baraza linaendelea kutekeleza jukumu lake la kuratibu, kuhamasisha na kuunganisha wadau wa uwezeshaji wananchi kiuchumi nchini kwa kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi kuhusu fursa zilizopo za mitaji, mafunzo ya ujasiriamali, usimamizi wa biashara na huduma za maendeleo ya biashara.

Alieleza kuwa utoaji wa elimu ya uwezeshaji ni sehemu ya mkakati wa NEEC wa kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanashiriki katika uchumi rasmi kwa kuanzisha na kukuza biashara endelevu zitakazoongeza kipato cha kaya na kuchochea maendeleo ya taifa.

Kuhitimishwa kwa mafunzo hayo katika Halmashauri ya Wilaya ya Laela kunahitimisha rasmi programu ya utoaji elimu iliyofanyika katika halmashauri zote nne za Mkoa wa Rukwa, ikiwa ni sehemu ya jitihada za NEEC za kuhakikisha wananchi wanapata maarifa na stadi zitakazowawezesha kutumia kikamilifu fursa za kiuchumi zinazotolewa na Serikali na wadau mbalimbali wa maendeleo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!