Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango amesema Serikali inatambua umuhimu wa sekta binafsi kama kichocheo cha kuimarisha sekta ya utalii hapa nchini hivyo imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kuleta mageuzi hususani katika sheria na maboresho ya sera ya bajeti ili kusaidia ukuaji wa sekta hiyo.
Makamu wa Rais amesema hayo leo tarehe 22 Oktoba 2022 wakati wa ufunguzi wa onesho la sita la kimataifa la utalii la Swahili (Swahili International Tourism Expo) linalofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Mlimani City Jijini Dar es salaam. Aidha ametaja hatua mbalimbali zinazochukuliwa na serikali ikiwemo kuboresha miundombinu ya huduma za utalii ambayo ni pamoja na ujenzi wa reli ya kisasa ya mwendokasi, kujenga na kukarabati barabara, viwanja vya ndege, kambi za watalii na kuongeza kasi ya Shirika la Ndege la Taifa ili kurahisisha safari za ndani ya Tanzania pia.
Aidha amesema Utalii ni miongoni mwa sekta zinazopewa kipaumbele na serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa bingwa wakuimarisha sekta hiyo baada ya Uviko-19. kupitia makala ya ubunifu ya The Royal Tour ambayo imepelekea matokeo chanya ya kuongezeka kwa watalii na mapato nchini.
Halikadhalika Makamu wa Rais ametoa wito kwa wawekezaji kuchangamkia fursa kubwa na ambazo hazijatumika hasa katika sekta ya utalii kutokana na Tanzania kutoa mazingira mazuri ya amani na utulivu kwa biashara na uwekezaji. Amewahimiza wawekezaji wote watarajiwa pamoja na washiriki wote wa onesho hilo kutumia maonesho hayo kama jukwaa la kupanua biashara na kuimarisha ushirikiano ili kuipeleka sekta ya katika viwango vipya na vya juu zaidi.
Kwa upande wake Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Pindi Chana amesema Wizara hiyo imeweka malengo ya kuongeza watalii wasiopungua milioni 5 pamoja na kuongeza pato la taifa la dola bilioni 6 ifikapo mwaka 2025. Aidha ameongeza kwamba Wizara imeendelea na jitihada kutangaza vivutio hususani katika ukanda wa kusini mwa Tanzania na kuwakaribisha wawekezaji na wadau wa utalii kuwekeza katika maeneo hayo.
Awali Waziri wa Utalii na Mambokale wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Simai Mohammed Said amesema ipo haja ya kuongeza jitihada na kuwekeza katika utalii wa urithi ikiwemo kufanya tafiti na kuhifadhi maeneo ya urithi yatakayopatikana kupitia tafiti hizo. Aidha amesema Wziara hizo za utalii bara na Zanzibar zitaendelea kushirikiana katika kufikia mapinduzi ya sekta hiyo hapa nchini.
Katika ufunguzi wa Maonesho hayo, Shirikisho la Chama cha waongoza watalii nchini wametoa zawadi ya kumtambua Rais Samia Suluhu Hassan kama muongozaji bora wa Watalii kwa mwaka 2022.
Onesho la Kimataifa la Utalii la Swahili kwa mwaka 2022 linahudhuriwa na washiriki zaidi ya 200 kutoka ndani na nje ya Tanzania, zaidi ya wanunuzi 100 wa kimataifa kutoka ndani na nje ya Afrika pamoja na wageni wa kibiashara 5,000. Onesho hilo lilianzishwa mwaka 2014 kwa lengo kutangaza vivutio vya utalii vinavyopatikana hapa nchini pamoja na fursa za uwekezaji.