
Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Same pamoja na watendaji wametakiwa kuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha wananchi wa maeneo yao kupima na kupata matibabu ya magonjwa ya ini mapema, ili kunusuru maisha ya waathirika wa maradhi hayo.
Agizo hilo limetolewa leo, Januari 31, na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo wakati wa Baraza la Robo ya Mwaka la Madiwani. Akizungumza katika kikao hicho, Mwenyekiti alisisitiza kuwa madiwani wana nafasi kubwa ya kufikisha elimu kwa wananchi ili kuongeza mwamko wa upimaji na matibabu ya ugonjwa huo.
“Madiwani ni viongozi wa karibu na wananchi, hivyo mna jukumu kubwa la kuwahamasisha kupima afya zao, hasa kwa magonjwa hatari kama ini. Tuwatie moyo kufika kwenye vituo vya afya ili kupata huduma mapema kabla ugonjwa haujafikia hatua mbaya,” alisema Mwenyekiti wa Halmashauri.
Hoja hiyo iliibuliwa na mmoja wa madiwani kwenye baraza hilo, ambaye alitaka kufahamu mpango wa halmashauri katika kukabiliana na changamoto za wagonjwa wa ini wilayani humo, kutokana na hatari ya ugonjwa huo.

Dkt. Alex P. Alexander, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Same, alieleza kuwa ugonjwa wa ini ni miongoni mwa magonjwa hatari na unahitaji juhudi za pamoja katika kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kupima mapema na kufuata matibabu.
“Ugonjwa wa ini ni hatari zaidi ukilinganishwa na magonjwa mengine kama UKIMWI, Mara nyingi dalili zake huonekana katika hatua za mwisho, hivyo ni muhimu wananchi kupima mara kwa mara ili kuanza matibabu mapema,” alisema Mganga Mkuu wa Halmashauri.
Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, ugonjwa wa ini unaweza kuzuilika kwa chanjo, lishe bora, na kuepuka matumizi ya pombe kupita kiasi. Halmashauri hiyo imeahidi kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuboresha huduma za upimaji na matibabu ya ugonjwa huo kwa wananchi wa Same.
