
Na Deborah Lemmubi-Mzawa Media-Dodoma.
Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe Dkt Ashatu Kijaji ameeleza kuwa Tanzania inatarajia kuwa na matukio makubwa ya kimataifa yatayofanyika nchini ambayo yanalenga kutangaza fursa mbalimbali za utalii zilizopo hapa nchini.
Waziri Dkt. Ashatu Kijaji ameyasema hayo leo Mei 15,2026 Bungeni Jijini Dodoma wakati akiwasilisha makadirio ya bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Na kuongeza kuwa, Tanzania inatarajia kutumia fursa za matukio manne yatakayofanyika hapa nchini ili kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo.
Ambapo ameyaainisha matukio hayo kuwa ni pamoja na Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (Inter Parliamentary Union Assembly-(IPU), utakaofanyika mwezi Oktoba 2026 jijini Arusha ambapo zaidi ya washiriki 1,500 na Maspika 183 kutoka nchi mbalimbali Duniani watahudhuria, tukio la utoaji wa tuzo za kimataifa za ubora kwenye sekta ya utalii duniani litakalofanyika mwezi Desemba mwaka 2026 ambapo washiriki zaidi ya 1,000 kutoka mabara ya Ulaya, Asia, Amerika ya kaskazini na kusini watahudhuria.
Pamoja naa Matukio mengine kama vile Shindano la Ulimbwende wa Dunia 2027 (Miss World) ambalo litahudhuriwa na takribani watu 20,000 pamoja na washindani 120 kutoka nchi mbalimbali Duniani na Mashindano ya mpira wa miguu kwa nchi za Afrika (AFCON 2027) ambapo Tanzania inatarajia kupokea wageni zaidi ya Milioni 1.8 na kuhusisha timu 24 kutoka Mataifa ya Afrika.
Aidha Dkt. Kijaji amesema kuwa Wizara imejipanga kikamilifu kutumia fursa za matukio hayo kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini kwa kushirikiana na wadau wa utalii kuandaa vifurushi maalumu vya safari za utalii kwa wageni watakaofika nchini kwa ajili ya matukio hayo ya kimataifa.
Katika mawasilisho hayo ya makadilio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo Dkt. Kijaji ameliomba Bunge kuidhinisha kiasi cha Shilingi Bilioni 334,345,870,000.
Ambapo Shilingi Bilioni 272,044,425,000 zitakwenda katika matumizi ya kawaida huku Shilingi bilioni 62,301,445,000 zitaelekezwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.









