Home Biashara TANZANIA NA  ZAMBIA KUENDELEA KUSHIRIKIANA KATIKA KUKUZA KIBIASHARA

TANZANIA NA  ZAMBIA KUENDELEA KUSHIRIKIANA KATIKA KUKUZA KIBIASHARA

Tanzania na Zambia zimekubaliana kuendelea kushirikiana katika kuibua fursa za biashara na kutatua mara moja changamoto zilizopo na zitakazojitokeza katika uwekezaji na biashara ili kukuza biashara na uwekezaji baina ya nchi hizo mbili.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) na Waziri wa Biashara na Viwanda wa Jamhuri ya Zambia Mhe. Chipoka Mulenga walipokutana na kujadiliana kuhusu masuala ya uwezeshaji, biashara na kukuza uchumi baina ya Tanzania na Zambia katika kikao kilichofanyika Agosti 3, 2022, Jijini Dar es Salaam.

Mawaziri hao walikutana kufuatia maagizo yaliyotolewa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mhe. Hakainde Hichilema, Rais wa Jamhuri ya Zambia katika kikao chao kilichofanyika Ikulu Dar es Salaam tarehe 2 Agosti 2022 ambapo waliagiza Mawaziri wa Biashara kukutana mara moja kujadili masuala ya biashara baina ya Tanzania na Zambia.

Dkt kijaji ameeleza kuwa miongoni mwa changamoto zinazofanyiwa kazi ni pamoja na ucheleweshaji wa kuruhusiwa magari ya Tanzania katika mpaka wa Tunduma Nakonde, Wafanyabiashara wadogo wakinyanganywa pasi zao za kusafiria, na Madereva Watanzania kuibiwa mizigo

Kwa upande wake Waziri wa Biashara na Viwanda wa Zambia amesema wanafanyia kazi changamoto zilizowasilishwa huku akisisitiza lengo ni kuimarisha biashara ndani ya Afrika

Katika kikao hicho, Mawaziri walikubaliana kufanya kikao cha pamoja ambacho kitajadili kwa kina masuala ya kibiashara na changamoto zilizopo baina ya Tanzania na Zambia. Waziri wa Zambia aliahidi ndani ya wiki mbili kuwasilisha mapendekezo ya tarehe za kikao hicho na ilikubalika kitanguliwe na kikao cha Sekta Binafsi.

Aidha Mawaziri hao walisisitiza kuendeleza ushirikiano ambao umekuwepo tangu enzi za Mhe. Mwalimu Julius Nyerere Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mhe. Keneth Kaunda, Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Zambia na sio kwa kushindana.

Vilevile, Mawaziri hao walikubaliana kuendeleza dhamira nzuri ya Waheshimiwa Marais wa nchi zote mbili ya kuondoa vikwazo na kuwezesha biashara na uwekezaji ili kukuza uchumi na hatimaye ajira kwa wananchi wa pande zote mbili.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!