
UMOJA Wa Waganga na Wakunga Wa Tiba Asili Tanzania (UWAWATA) umewataka wanachama wake kusajiriwa ili wapate leseni kutoka Wizara ya Afya waweze kuaminiwa na jamii katika tiba wanazotoa kwa wagonjwa.
Wito huo umetolewa jana na Wadau wa Tiba Asili wilayani Misungwi kwenye mafunzo yao ya kujengeana elimu juu ya namna ya kuboresha utoaji wa huduma zao kwa ufanisi kwenye jamii.
Katibu Mkuu wa UWAWATA Taifa Lucas Mlipu alisema umoja wao unawahimiza wanachama wake wote kuhakikisha kuwa wanasajiriwa na umoja wao na kupata leseni kutoka Wizara ya Afya ili waweze kuaminiwa na kufanya kazi sehemu yoyote hapa nchini bila ya vikwazo.
Alisema vilevile wanayo mitaala ya kuwafundisha wanachama wao namna bora ya utoaji huduma za tiba na ukunga ili kuwezesha wagonjwa kupona na kuondokana na changamoto zinazowakabili kwa wakati.

Wakati huo huo waganga na wakunga wa Tiba Asili 34 wa UWAWATA walipatiwa leseni kutoka Wizara ya Afya katika washa hiyo iliyoendeshwa kwa siku mbili wilayani Misungwi.
Mmoja wa wanachama wa UWAWATA aliyepata leseni ya kuendeshea shughuli yake Hussein Mzega toka Fera alishukuru kuweza kupata leseni kwani itamuondolea mashaka na kumuongezea Imani kwenye jamii.
Alisema vilevile kuwa kupitia mafunzo aliyoyapata kwenye washa hiyo yamemuongezea maarifa ya ufanyaji kazi zake vizuri zaidi.
Naye Najim Hussein Salum kutoka Kahama alisema amefurahi kupata leseni hivyo ataweza kusaidia jamii vizuri zaidi huku akipongeza elimu aliyopata kuwa ni msaada mkubwa katika ufanyaji wa kazi zake
