Home Kitaifa IDADI YA VISIWA VINAVYOKODISHWA ZANZIBAR YAFIKIA KUMI NA SABA(17)- MHE.SORAGA

IDADI YA VISIWA VINAVYOKODISHWA ZANZIBAR YAFIKIA KUMI NA SABA(17)- MHE.SORAGA

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nchi Afisi ya Rais – Kazi, Uchumi na Uwekezaji Mudrik Ramadhan Soraga wakati akijibu swali la mwakilishi wa Jimbo la pandani Mhe Prof. Omar Said Fakihi kuhusu maendeleo ya mchakato wa Serikali katika ukodishaji wa visiwa vidogo vidogo kwa ajili ya Uwekezaji, katika kikao cha kumi na tatu cha Baraza la kumi la Wawakilishi huko Chukwani Mkoa wa Mjini Magharib Unguja

Amesema Serikali mnamo mwishoni mwa miaka ya 80 Serikali ilifungua milango katika sekta ya utalii kwa lengo la kukuza uchumi wa nchi hivyo serikali ya awamu ya nane iliamua kuvikodisha Visiwa Kumi (10) kwa awamu ya mwanzo kwa ajili ya uwekezaji na kuendelea kuvitangaza visiwa vyengine 10 kwa Uwekezaji ambapo visiwa 7 kati ya hivyo vya Awamu ya Pili tayari wameshajitokeza wawekezaji na kufanya idadi ya Visiwa vyote vilivyokodishwa kufikia 17 hadi kufikia mwezi Septemba 2022.

Waziri Soraga amefahamisha kuwa awali Serikali ilikuwa ikiangalia zaidi mapato yatokonayo na kodi ya ukodishwaji wa ardhi (Land Lease) katika visiwa vinne vilivyokodishwa mnamo mwaka 2000 ambavyo ni Mnemba, Chapwani, Changuu na Bawe lakini sasa Serikali inatarajia kukusanya Dola za Kimarekani Milioni 19.8 kama malipo ya awali na Mtaji wa kiasi cha Dola za Kimarekani Milioni 442.5 ambazo zitasaidia kwa kiasi kikubwa kuinua Uchumi wa Nchi na Wananchi wa Zanzibar.

“Serikali haijasita kuvikodisha visiwa vyengine, bali Serikali inaendelea kuvitangaza visiwa ambavyo vina muonekano wa kuvutia wawekezaji kwa mujibu wa masharti yanayowekwa.” Alisema Soraga

Akielezea vigezo vilivyowekwa kupitia Mamlaka ya Kukuza uwekezaji Zanzibar (ZIPA) kwa wawekezaji wanaotaka kukodi visiwa hivyo amesema ni pamoja na uwezo wa mwekezaji katika kuhifadhi mazingira ya kisiwa, uwezo wa kifedha, ushirikiano baina ya mwekezaji na jamii, aina ya uwekezaji unaotaka kufanyika pamoja na malipo ya awali ya ukodishwaji wa Visiwa (Kilemba) ambapo hadi sasa malipo ya awali ya Dola za Kimarekani Milioni 11.1 yameshalipwa kwa baadhi ya Visiwa vilivyokamilisha vigezo hivyo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!