Home Biashara DKT.KIRUSWA AWATAKA WACHIMBAJI WADOGO WA MADINI KWENDA KUJIFUNZA NZEGA

DKT.KIRUSWA AWATAKA WACHIMBAJI WADOGO WA MADINI KWENDA KUJIFUNZA NZEGA

Na Asteria Muhozya – NZEGA

Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa amewataka Wachimbaji Wadogo wa Madini nchini kujifunza kutoka kwa wachimbaji wa Wilaya ya Nzega kutokana na uthubutu walioufanya kuanzisha maabara za kisasa za kupima mchanga wa madini kabla ya kuchenjuliwa ikiwemo kuanzisha viwanda vya kuchenjua dhahabu.

Dkt. Kiruswa ameyasema hayo kwa nyakati tofauti katika ziara yake Wilayani Nzega ambapo ametembelea Kiwanda cha Kati cha Kuchenjua Dhahabu cha Savanna Reef kinachomilikiwa na Mtanzania Pirbaksh Rasulbaksh na Kampuni ya Kasala Gold Mine yenye kiwanda cha kuchenjua dhahabu inayomilikiwa na Mtanzania Daudi Mwita, huku kampuni zote zikiwa zimeanzisha maabara za kupima mchanga wa madini kupata usahihi wa viwango vya dhahabu kabla ya kuchenjuliwa.

Hatua ya kuanzishwa kwa maabara hizo inafuatia malalamiko ya kuibiwa kaboni kwenye viwanda cha kuchenjua dhahabu kutoka kwa wachimbaji, hivyo ofisi ya Madini mkoani humo ikaweka utaratibu wa kuhakikisha mchanga wa dhahabu unapimwa maabara kabla ya kuchenjuliwa.

Akizungumza katika kiwanda cha Savanna Reef, Naibu Waziri amesema tayari kiwanda hicho kimenunua mtambo wa kuchoronga miamba na kipo katika mpango wa kuanzisha mgodi wa uchimbaji madini. Kufuatia hali hiyo, amewataka wachimbaji wengine kujifunza kiwandani hapo kuhusu namna bora ya utunzaji wa mazingira, uchenjuaji wa kisasa na namna ya kuanzisha migodi.

‘’ Nimeona, alichokifanya ni kikubwa na amefika katika hatua kubwa. Kama Serikali niko hapa kuwapa moyo wanaofanya vizuri, ninawapongeza mkoa wa Tabora kwa maendeleo haya na ninapenda kuwaona wengine wakijifunza kupitia hapa,’’.

Aidha, amemtaka mwekezaji wa Savvana Reef kuwasiliana na Ofisi ya Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Tabora kwa ajili ya kupatiwa utaratibu wa kushughulikia masuala yanayohusu wajibu wa kampuni kwa jamii. Pamoja na hayo, awali, mwekezaji huyo amemwomba Naibu Waziri kuifikiria kampuni hiyo kwa kuipatia eneo linalomilikiwa na Serikali kwa ajili ya kuchimba madini . Akijibu ombi hilo, Naibu Waziri amemweleza mwekezaji huyo kuwasilisha maombi kwa njia ya maandishi.

Pia, Naibu Waziri Dkt.Kiruswa amempongeza Daudi Mwita kwa kuanzisha maabara hiyo na kuwataka wachimbaji kuitumia kupima madini yao kabla ya kuchenjuliwa na kutoa wito kwa mikoa jirani kuitumia maabara hiyo.

Amesema Dira ya Wizara ni kukuza uchimbaji mdogo, hivyo kutokana na uthubutu uliooneshwa na watanzania hao ni dhahiri kuwa kupitia dira hiyo itasaidia kuwakuza wachimbaji wengine.

Katika hatua nyingine, Chama Cha Wachimbaji wa Madini Mkoa wa Tabora (TABOREMA) kimeikumbusha Wizara kuhusu ombi la kuanzishwa kwa Benki ya Madini lililotolewa na Shirikisho la Vyama Vya Wachimbaji wa Madini Tanzania (FEMATA) wakati wa Mkutano wa Nne (4) Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini uliofanyika mwezi Februari, 2022.

Akiwasilisha taarifa kwa niaba ya Chama hicho kwa Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven, Joseph Mabondo amesema licha ya jitihada kubwa zilizofanywa na Wizara za kuwaunganisha wachimbaji na Taasisi za Fedha, bado baadhi ya benki zinasita kutoa mikopo kwa wachimbaji wadogo hivyo uwepo wa benki hiyo utawasaidia wachimbaji kupata mikopo ambayo watarejesha kwa utaratibu.

Aidha, katika ziara hiyo, wachimbaji wamemwomba Naibu Waziri kusaidia tatizo la ukosefu wa nishati ya umeme katika maeneo ya migodi ikiwemo miundombinu ya barabara na kueleza kuwa, ukosefu wa umeme unasababisha gharama za uendeshaji kuwa kubwa na hivyo kupelekea kupungua kwa uzalishaji.

Kwa upande wake, Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Tabora Mayingi Makolobela licha ya kupongeza ushirikiano anaopatiwa na wadau wa madini mkoani humo, amezuia kuwepo kwa watoto wadogo katika maeneo yenye shughuli za migodi badala yake ametaka watoto hao kupatiwa haki yao ya msingi ya kuwa shuleni kipindi wazazi wanapofanya shughuli zao za madini.

Pia, amesisitiza kwa mdau yoyote anayehitaji kupata taarifa zinazohusu biashara ya madini kufika katika Ofisi hiyo kwa ajili ya kupatiwa taratibu badala ya kufanya shughuli zao kinyume na taratibu zilizowekwa.

Awali, kabla ya kuanza ziara hiyo, Naibu Waziri Dkt. Kiruswa amekutana na Mkuu wa Wilaya ya Nzega Kamishna Msaidizi wa Polisi Advera Buhimba ambapo amemweleza malengo ya ziara hiyo. Pia, Dkt.Kiruswa amekutana na wafanyabiashara wa Madini katika Soko la Madini Nzega ambapo wamewasilisha changamoto zao.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!