
Rais wa Chama cha Wakunga Tanzania (TAMA), Dk. Beatrice Mwilike, amesema kuwa kwa sasa Afrika inakabiliwa na upungufu wa takriban wakunga 460,000, hali ambayo inaendelea kuweka maelfu ya mama na watoto wachanga katika hatari kila mwaka.
Pia amesema TAMA, kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya afya, kimetoa wito wa uwekezaji wa haraka katika taaluma ya ukunga ili kukabiliana na uhaba unaoongezeka wa wataalamu wenye ujuzi na kuboresha huduma za afya kwa mama na watoto wachanga nchini kote.

Hayo ameyabainisha leo, Aprili 20, 2026, jijini Dar es Salaam, Dk. Beatrice wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wakunga 2026, ambayo huadhimishwa duniani kote kila Mei 5 chini ya kaulimbiu ya mwaka huu, “Wakunga Milioni Moja Zaidi.”
“Wakati mzigo wa kazi unaopendekezwa katika maeneo mengine ya bara ni mkunga mmoja kuhudumia takriban mama wanane kwa siku, nchini Tanzania mkunga mmoja anaweza kuhudumia hadi mama 20 kwa siku. Pengo hili linaweka shinikizo kubwa kwa wakunga na linaathiri ubora wa huduma zinazotolewa kwa mama na watoto wachanga,” ameeleza.
Amesema TAMA, kwa kushirikiana na wadau, inapanga kukusanya shilingi bilioni moja kupitia mbio za nusu marathoni za wakunga pamoja na shughuli mbalimbali za uhamasishaji. Kampeni hiyo pia itajumuisha maonesho ya afya ya jamii, huduma za kufikia wananchi (outreach) na mafunzo ya kitaaluma yenye lengo la kuimarisha ujuzi wa ukunga na kuonesha mchango muhimu wa taaluma hiyo katika kuokoa maisha.
Kulingana naye, fedha hizo zitasaidia kuongeza uelewa wa umma kuhusu umuhimu wa wakunga katika kuhakikisha uzazi salama, kuimarisha ushirikiano kati ya wadau katika huduma za afya ya mama na mtoto, na kutetea sera zinazounga mkono taaluma hiyo pamoja na kuboresha mazingira ya kazi.
“Tanzania inaunga mkono wito wa kimataifa kwamba dunia inahitaji wakunga milioni moja zaidi. Kila mtu ana nafasi ya kushiriki kama mshirika, mfadhili au mtetezi katika kuimarisha huduma za afya ya mama na mtoto katika jamii zetu,” amesema.
Mratibu wa Kanda ya Afrika Mashariki na Kati kutoka Chama cha Wakunga Canada, Stephano Simba, amesema kuwa kwa kipindi cha miaka saba iliyopita, taasisi yake imekuwa ikiunga mkono mipango ya mafunzo ya ukunga na kuchangia kuboresha mitaala ya taaluma hiyo katika ukanda huu.
“Sasa tunaweka mkazo zaidi katika kuimarisha uwezo wa TAMA kama chama cha kitaaluma ili kiweze kuendelea kuwasaidia wakunga kwa ufanisi,” amesema.
Kwa upande wake, Ofisa Mkuu wa Uuguzi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Joyce Munga, amehamasisha wananchi na taasisi kushiriki katika mbio hizo na kuunga mkono juhudi za uchangishaji fedha zinazolenga kuboresha huduma za afya ya uzazi, mama, watoto wachanga, watoto na vijana nchini kote.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi na Ukunga, Ziada Sellah, amesema serikali inaendelea kujitolea kushirikiana kwa karibu na wadau ili kukabiliana na uhaba wa wakunga na kuimarisha utoaji wa huduma.
Amesisitiza kuwa kuwawezesha wakunga ni muhimu katika kuboresha afya ya familia na kupunguza vifo vya mama na watoto wachanga nchini kote.








